Afya

Serikali yaajiri watumishi 6,180 wa kada ya afya katika halmashauri

Na Mwandishi wetu
Jumla ya waombaji 6,180 kati ya 14,647 wenye sifa za kuajiriwa kwenye kada mbalimbali za afya katika Mamlaka za Serikali za Mitaa wamefanikiwa kuajiriwa na serikali kufuatia kukamilika kwa mchakato wa ajira wa watumishi hao.
Kauli hiyo imetolewa jana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.Selemani Jafo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma.


Mhe.Jafo aliongeza kuwa jumla ya waombaji 24,891 waliomba nafasi za ajira za kada mbalimbali katika Mamlaka za Serikali za Mitaa wakiwemo madaktari, wafamasia, wataalam wa Maabara, Wauguzi, Tabibu, wahudumu wa Afya na Wataalamu wengine wa sekta ya Afya.
Kufuatia kukamilika kwa zoezi hilo, Mhe.Jafo amewataka waombaji wote waliofanikiwa kupangiwa katika vituo mbalimbali vya Mamlaka za Serikali za Mitaa kuripoti katika vituo vya kazi walivyopangiwa katika muda wa siku 14 kuanzia jana.
“Watakaoshindwa kuripoti katika vituo vyao vya kazi ndani ya siku 14 kuanzia jana watambue kuwa nafasi zao zitajazwa na waombaji wengine haraka iwezekanavyo,” alisema.

Aidha Waziri Jafo aliongeza kuwa waombaji wote waliofanikiwa kupata ajira wanatakiwa kuwasilisha vyeti vyao halisi vya kidato cha nne, sita, chuo, NACTE, na vyeti halisi vya usajili wa mabaraza ya kitaalamu kwa ajili ya kuhakikiwa na mwajiri kabla ya kupewa barua ya ajira.
“Naomba niwatahadharishe mapema waombaji wote waliopata ajira kuwa hakutakuwa na nafasi ya kubadilisha vituo vya kazi walivyopangiwa na watambue kuwa wale wote watakaoshindwa kuripoti katika muda uliopangwa nafasi zao zitajazwa na waombaji wengine wa kada husika,” alisisitiza.
Kwa mujibu wa Waziri Jafo, kuajiriwa kwa watumishi hao wapya katika kada ya afya ni muendelezo wa kibali cha ajira za kada ya afya 3152 ambacho kilitolewa mwezi julai, 2017 kwa lengo la kukabiliana na changamoto za uhaba wa watumishi katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini.
Alisema kuwa mgawanyo wa watumishi hao wapya katika Mamlaka za Serikali za Mitaa umezingatia kuwapeleka wataalamu hao katika halmashauri zenye hospitali, vituo vya afya na Zahanati zilizokamilika kujengwa lakini zilikuwa hazifanyi kazi ipasavyo kutokana na kukosa watumishi.
Aidha mgawanyo umezingatia kupeleka wataalamu kwenye vituo vya afya 210 vilivyoboreshwa katika halmashauri mbalimbali ili kuziwezesha kutoa huduma zilizokusudiwa.
Mhe.Jafo amesema kuwa mgawanyo pia umezingatia halmashauri zenye zahanati zinazoongozwa na wahudumu wa afya na zile zinazoongozwa na wauguzi na pia halmashauri zenye uhaba mkubwa wa watumishi kwa mujibu wa taarifa ya Mahitaji wa watumishi katika vituo vya kutolea huduma za afya kulingana na uzito wa kazi.
Aidha Waziri wan chi alitoa shukrani kwa Mhe.Dkt John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuipatia Ofisi ya Rais TAMISEMI kibali cha kuajiri watumishi hao wapya.

Bofya hapo chini kuangalia

http://tamisemi.go.tz/announcement/orodha-ya-majina-ya-watumishi-wa-afya

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *