mikoani

Serikali yaamuru kituo cha kukabiliana na COVID-19 kubadilishwa

Na.Majid Abdulkarim, Singida

Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia masuala ya Afya katika Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dkt Dorothy Gwajima, ameelekeza Manispaa ya Singida kubadilisha  kituo cha matibabu kwa ajili ya wagonjwa watakaobainika  kuwa na Covid19 (CORONA) kutokana barabara inayoenda huko miundombinu yake kuhitaji marekebisho kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha hivyo kuleta changamoto ya kupitika kwake.

Maelekezo hayo ameyatoa leo katika ziara yake ndani Manispaa ya Singida akikagua matayarisho ya vituo kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa husika ikiwemo Kituo cha Afya Sokoine mkoani hapa.

Katika ziara hiyo amebaini Kituo cha Afya Sepuka kilichokuwa kimetengwa kwa Manispaa hiyo miundombinu yake inahitaji kurekebishwa kufuatia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha.

Hivyo, Dkt.Gwajima ameagiza mkoa huo utenge eneo mbadala na kutoa taarifa mara moja ndani ya saa 24 ni wapi kituo kitakapokuwa kituo kingine cha kutolea huduma kwa wagonjwa watakao bainika kuwa na ugonjwa huo.

Aidha, Kwa kuongezea Dkt. Gwajima amewataka Waganga Wakuu wote wa Mikoa na Halmashauri kuhakikisha maeneo yote yaliyotengwa yanapitika .

“Wakurugenzi wa Halmashauri hakikisheni maeneo korofi ya barabara yanadhibitiwa kwa kuomba ushirikiano wa TARURA ili kuwezesha shughuli za kijamii kuendelea vyema” ameelekeza Dkt.Gwajima.

Dkt Gwajima amewapongeza watumishi wote wa sekta ya afya,  wananchi na wadau wote kwa ujumla kwa jinsi wanavyojitoa katika kuhakikisha nchi inashinda vita dhidi ya Covid19 haraka iwezekavyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *