Habari za Wizara

Serikali yafanya Mapitio ya Sera ya Ugatuzi wa Madaraka

Zulfa Mfinanga

SERIKALI imeanza kufanya uchambuzi wa kina juu ya kazi mbalimbali za serikali zinazofanyika katika dhana ya ugatuzi wa madaraka kwa lengo la kuboresha sera mpya ya ugatuzi wa madaraka ili iwe kwenye mfumo wa kisheria.

Hayo yamezungumzwa leo na Naibu Katibu Mkuu elimu kutoka Ofisi ya Rais-TAMISEMI Tixon Nzunda kwenye warsha ya mapitio ya sera ya ugatuaji wa madaraka na majukumu ya Wizara, Idara pamoja na Wakala wa serikali jijini Dodoma.

“Kazi kubwa inayofanyika hapa ni kuboresha mfumo huu uwe mfumo wa kisheria, mfumo ambao upo ndani ya sera lakini  pia uweze kueleweka katika ngazi zote za serikali” Alisema Naibu Katibu Mkuu Nzunda.

Awali akifungua warsha hiyo Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Profesa Faustine Kamuzola amewatoa hofu wananchi na kusema kuwa hakutakuwa na  ukinzani wowote kati ya sera mpya ya ugatuzi wa madaraka inayotarajiwa kutungwa pamoja na hii inayotumika kwa sasa.

“Hakuna ukinzani, tunataka kuwa na sera ya ugatuzi wa madaraka ambayo inazingatia mazingira halisi ya hivi sasa katika suala zima la uchumi kwa kuzingatia kuwa jamii yetu imedhamiria kusonga mbele haraka na kufikia uchumi wa kati kwa muda mfupi” Alisema Profesa Kamuzola na kuongeza.

“Sera hii ya sasa imeleta mafanikio mengi kwani wananchi hususani waliopo ngazi ya chini wamefahamu majukumu yao, lakini pamoja na mafanikio hayo tunataka kuangalia pia changamoto zilizojitokeza ili kuzifanyia marekebisho kwa lengo la kuimarisha huduma kwa jamii”

Aidha Profesa Kamuzola ameshauri kuwepo kwa mkakati  wa mawasilianao kuanzia ngazi za chini za utendaji ili kila mmoja kwa nafasi yake afahamu kwa undani dhana halisi ya sera hii ili kuweza kufanikisha malengo yaliyokusudiwa.

Mshauri na Mtafiti kutoka Chuo Kikuu Mzumbe Aloyce Maziku amesema ushiriki wa chuo hicho katika mapitio ya sera mpya unatokana na wao kushiriki kwenye utungaji wa sera mbalimbali, tafiti na maboresho kwenye ngazi ya Serikali za Mitaa.

“Sisi kama Chuo Kikuu Mzumbe kwa kushirikiana na wadau mbalimbali tutaangali changamoto zilizopo kwa lengo la kuboresha sera mpya ijayo ambayo inalenga kutatua  changamoto za sasa na kuzingatia mahitaji za sasa hususani sera ya uchumi wa viwanda” Alisema Maziku.

Mapitio ya sera ya ugatuaji wa madaraka ya mwaka 1998 yanafanywa na Taasisi ya DEGE kwa kushirikiana na Chuo Kikuu Mzumbe ambapo Taasisi ya REPOA inafanya mapitio ya majukumu ya Wizara, Idara pamoja na Wakala wa Serikali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *