Elimu

Serikali yagawa Pikipiki 2894 kwa Waratibu Elimu Kata nchini

Na Mathew Kwembe Dar es salaam

Serikali imezindua zoezi la usambazaji wa pikipiki 2,894 kwa Waratibu Elimu kata nchini kwa kutoa wito kwa Maafisa Elimu wa Wilaya kuhakikisha kuwa pikipiki hizo zinawafikia walengwa hao.

Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa funguo za pikipiki hizo na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako, kwa niaba ya Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa amewataka Maafisa wa Elimu kuhakikisha kuwa pikipiki hizo aina ya Honda zitumiwe na Waratibu Elimu kata.

Alisema kuwa serikali ya Awamu ya tano chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt John Pombe Magufuli imelipa uzito suala la utoaji wa elimu bora nchini ndiyo maana serikali imeamua kuanzisha mpango wa kutoa elimu bila malipo.

“Ni matumaini yangu baada ya serikali kukubali kutoa pikipiki hizi suala la usimamizi wa elimu katika kata zenu litaenda kufanyika vizuri bila visingizio vyovyote,” alisema.

Mhe.Jafo alisisitiza kuwa  serikali inaenda kuwapatia waratibu wa elimu kata pikipiki hizo na kamwe pikipiki hizo zisitumiwe kwa ajili ya shughuli nyingine zozote mbali na ufuatiliaji na usimamizi wa shule katika kata husika.

“Napenda kulisisitiza jambo hili, pikipiki hizi siyo za kuendea kwenye viti virefu, na pia zisitumike kufanyia shughuli ya bodaboda,” alisema Mhe.Jafo.

Aidha aliwataka Maafisa Elimu Wilaya kuhakikisha kuwa pikipiki hizo aina ya Honda ndiyo zitakazogawiwa kwa waratibu elimu kata na si vinginevyo.

“Sitaki kusikia kuwa waratibu wa elimu kata wamegawiwa pikipiki za aina nyingine badala ya aina hii ya Honda tunazozigawa leo,” alisema.

Alisema serikali inalenga kupandisha ubora wa elimu katika ngazi ya kata, hivyo amewaagiza wakurugenzi wa halmashauri kuhakikisha kuwa pikipiki hizo zinapatiwa huduma ya mafuta bure katika kipindi cha miezi sita.

 

Naye Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako alisema kuwa pikipiki hizo zilinunuliwa na Wizara yake kupitia programu ya Lanes ambapo serikali imehakikisha kuwa pikipiki hizo ina vifaa vyote vya usalama barabarani.

Alisema kuwa ni matarajio yake kuwa pikipiki hizo zitawawezesha waratibu elimu kata kuboresha ubora wa elimu katika kata kwa kufanya ufuatiliaji wa mara kwa mara katika shule zao.

Alisema kuwa hatarajii kuona wanafunzi wengi wanaendelea kupata daraja la sifuri, na kamwe shule zisiwe vituo vya kulea watoto badala yake kata ziimarishe usimamizi wa elimu.

Mapema Mwakilishi wa wadau wa Maendeleo Bibi Susan Steven alisema kuwa wao kama wadau wa maendeleo  wamefurahishwa na hatua ya serikali kushirikiana nao katika kuleta maendeleo ya elimu Tanzania.

 

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *