Habari za Wizara

Serikali yahaidi ununuzi wa Ultra Sound kwenye vituo vya afya nchini.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Josephat Senkamba Kandege akijibu Maswali leo Bungeni Jijini Dodoma.

Na. Angela Msimbira BUNGE -DODOMA

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Josephat Senkamba Kandege amesema Serikali imejiwekea mikakati wa kuhakikisha vituo vyote vya afya vilivyojengwa nchini vinakuwa na wataalam, vifaa vya kutosha kikiwemo kipimo cha Ultra-Sound ili kutoa huduma bora za afya kwa wananchi

Akijibu swali Bungeni leo lililotaka ufafanuzi juu ya mkakati wa Serikali wa kununua kipimo cha Ultra Sound katika Kituo cha afya cha Ujiji Mkoani Kigoma Mhe. Kandege amesema  katika mwaka wa fedha 2018/2019 Serikali imeidhinishiwa  zaidi ya shilingi milioni 15  kwa  Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma Ujiji kupitia mradi wa malipo kwa ufanisi kwa ajili ya ukarabati wa chumba kinachotumika kwa huduma ya mionzi na shilingi milini 45 kwa ajili ya ununuzi wa Ultra Sound

Anafafanua kuwa huduma ya Ultra Sound katika Mkoa wa Kigoma kwa sasa inapatikana katika Hospitali ya Mkoa ya Maweni na Hospitali Teule ya Batist kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wanaohitaji huduma hiyo.

Mhe. Senkamba amesema Serikali inatambua umuhimu wa kifaa cha Ultra Sound katika Vituo vya Afya vyote nchini na tayari imepeleka fedha Bohari ya dawa (MSD) kwa ajili ya ununuzi wa kifaa hicho ili kuhakikisha vituo vyote vinapokamilika vinakuwa na huduma ya Ultra Sound.

Aidha amesema ni azma ya Serikali kuhakikisha vituo vyote vya afya  vinavyojengwa  vikikamilika  viweze kutoa huduma ya Ultra Sound, kuwa na wataalam wa kutosha pamoja na kuwa vifaa vya kutosha ili  wananchi wapate huduma bora na kupunguza kero za afya katika jamii.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *