Miundombinu

Serikali Yaigiza TARURA Kujenga Barabara kwa Wakati

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Selemani S. Jafo (Mb) akitoa maelekezo kwa Watendaji wa TARURA nchini kuacha kutengeneza barabara kama bado haijatengewa bajeti ili kuondoa adha kwa wananchi. Kulia kwake ni Dkt. Binilith Mahenge Mkuu wa mkoa wa Dodoma na kushoto ni Mratibu wa TARURA Mkoa wa Dodoma Mhandisi, Lusako Kilebwe

Na Fred Kibano
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Seleman Jafo, amepiga marufuku tabia ya Wakala wa barabara mijini na vijijini TARURA, kuchonga viboksi barabarani wakati wa kuziboresha barabara hizo na kuacha mashimo kwa muda mrefu na kuwa kero kwa watumiaji.

Waziri Jafo ameyasema hayo leo jijini Dodoma, wakati wa ziara ya kukagua miradi ya uboreshaji wa barabara za ndani na nje ya jiji, zinazotekelezwa na Serikali kukabiliana na kero za foleni za barabarani.

Jafo amesema kuwa kuna tabia imejengeka ya TARURA wakati wa kurekebisha miundo mbinu ya barabara wamekuwa wakichonga viboksi na kuviacha kwa muda mrefu hali inayoleta usumbufu kwa watumiaji wa barabara hizo, na kusababisha ajari hasa kipindi hiki cha mvua.

“Niagize Tarura tabia ya kuanza kuchonga barabara mnachonga viboksi wakati hamjajiandaa kuanza ukarabati na mnaacha viboks hivyo mwezi mmoja miezi miwili hiyo tabia muache, maeneo mengi nimepita nimeona, nikipita na kuona tena mkoa wowote meneja atakuwa hana kazi.” amesema Jafo.

Aidha, Jafo amemuagiza Wakala wa TaARURA Mkoa wa Dar es salaam hadi kufika alhamisi wiki hii awe ametoa maelezo kwanini mkoa huo umekuwa na mashimo mengi ambayo yamekaa muda mrefu bila kutengenezwa na kuagiza ndani ya muda huo mashimo hayo yawe yametengenezwa kwani yanaleta adha kubwa kwa watumiaji wa barabara mkoani humo.

“Pia niagize Meneja wa TARURA mkoa wa Dar es salaam ndani ya siku tatu awe aniletee maelezo kwanini ndani ya mkoa wake amechonga mashimo na kukaa mda mrefu bila kutengeneza na anieleze kwanini kwenye mashimo hayo hajaweka rami na wananchi wanazidi kuteseka” amesema Jafo

Amesema kuwa kama tarura haijakamilisha na kuwa tayari kuanza matengenezo kwanini wachonge mashimo hayo? Pia alipiga marufuku tabia wa wakandarasi kuweka vifusi wakati wa matengezezo na vifusi kukaa mda mrefu huku vikiendelea kuleta kero kwa watumiaji na waache tabia hiyo.

Kwa upande wa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Binilith Mahenge alimpongeza waziri Jafo kwa kufuatilia kwa makini miradi hiyo, na kuahidi kuitekeleza kwa umakini na kwa wakati ili adhima ya serikali iweze kutimia.

Naye Mratibu wa TARURA Mkoa wa Dodoma Mhandisi, Lusako Kilebwe, amesema kuwa ukarabati wa barabara hizo za ndani na nje ya mji ni moja ya mbinu za kupambana na msongamano wa magari katika Jiji ili liwezekuendana na hadhi ya kuwa Jiji.

Mhandisi Lusako amesema kuwa wao kama Tarura changamoto wanazokumbana nazo ni utumiaji mbaya wa wananchi katika miondombinu Hiyo na kusababisha kuharibika mapema.

“Sisi kama Tarura tunajitahidi kuboresha miundombinu na kukarabati lakini chanangamoto zinazotukabili na utumiaji wa miondombinu hiyo tunajenga barabara zenye taa lakini watu wanazigonga nguzo za barabarani watu wanaendesha huku wamelewa na wanazingonga na kuharibu.

Miongoni mwa barabara alizokagua Waziri wakati wa ziara hiyo ni pamoja na barabara ya VETA, barabara ya Ilazo, Swaswa na barabara ya martin Luther inayounganisha makazi ya Mhe Waziri Mkuu na mtaa wa Area D Jijini Dodoma na kuridhishwa na hatua zinazoendelea.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *