Habari za Kiuchumi/Kilimo

Serikali Yakabidhi Mashine za Kutengeneza Vyeti vya Walipa Kodi

 

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhandisi Joseph Nyamhanga akimkabidhi Kamishna wa TRA Bw. Charles Kichere sehemu ya mashine 13 za  kutengeneza vyeti vya walipa kodi (Taxpayers Mobile Kits) zenye thamani ya shilingi milioni 167,553,376.00 zitakazotumiwa na Maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania kutoa huduma kwenye vituo vya kutolea huduma za Biashara na Uwekezaji katika Halmashauri zote za Mikoa ya Dodoma na Kigoma katika ofisi za OR – TAMISEMI Jijini Dodoma. Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu OR-TAMISEMI (ELIMU) Tixon Nzunda.

Na Fred Kibano

Serikali imekabidhi mashine 13 za kutengeneza vyeti vya walipa kodi (Taxpayers Mobile Kits) zenye thamani ya shilingi milioni 167,553,376.00 zitakazotumiwa na Maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania kutoa huduma kwenye vituo vya kutolea huduma za Biashara na Uwekezaji katika Halmashauri zote za Mikoa ya Dodoma na Kigoma Jijini Dodoma.

Akipokea msaada huo wa mashine 13 kutoka Serikali ya Denmark kupitia Mradi wa Kuboresha Mazingira ya Biashara nchini (LIC – Local Investment Climate) zilizokabidhiwa na Mwakilishi wa Mradi huo nchini, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhandisi Joseph Nyamhanga amesema Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya huduma za biashara ili kumpunguzia mfanyabiashara na wajasiriamali gharama za uendeshaji na uendelezaji wa biashara.

Mhandisi Nyamhanga amesema jumla ya vituo 13 vya biashara vimejengwa katika Mikoa ya Dodoma na Kigoma ambapo wadau wote wanaohusika na mchakato wa utoaji leseni za biashara watatoa huduma katika eneo moja.

Aidha, Nyamhanga amesema uboreshaji wa utoaji wa huduma katika vituo hivyo kutapunguza urasimu, kuongeza ufanisi na uwajibikaji, kupanua wigo wa walipa kodi na kuongeza mapato ya Serikali kama ilivyo azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.

Kwa upande wake Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, Bw, Charles Kichere amesema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Ofisi ya Rais TAMISEMI ni wabia wakubwa katika ukusanyaji wa mapoto nchini na ndiyo maana ushirikiano huo upo ambapo kwa hivi sasa vitambulisho vya wafanyabiashara wadogo (machinga), kodi za majengo na utambuzi wa wadau kwenye vitalu vya biashara unafanywa kwa pamoja.

Amesema TRA inaangalia namna ya kuwawezesha wafanyabiashara kwa siku 90 baada ya kufungua na kuanza kufanya biashara zao na hilo litasaidia kuwalea wafanyabiashara wadogo lakini pia vituo vya biashara vitasaidia kutoa elimu kwa walipa kodi.

Naye, Kiongozi wa Mradi wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji Bw. Donald Liya amesema lengo la kununua mashine hizo ni baada ya kubaini kuwepo kwa biashara ambazo hazijarasimiwa katika maeneo mbalimbali na hivyo kupelekea ukosefu wa mapato na takwimu za kibiashara kwa maendeleo ya Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini.

Akitoa maelezo baada ya makabidhiano, Naibu Katibu Mkuu (ELIMU) Ofisi ya Rais TAMISEMI Tixon Nzunda amesema Mradi wa wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji una maeneo mengi ya utekelezaji kama vile suala la kuimarisha mazingira ya ukuaji wa biashara, uboreshaji kongani katika biashara (value chains) kama masoko, miradi ya kilimo, viwanda vidogo, miradi ya kuwaimarisha wafanyabiashara wadogo

Awali akitoa maelezo akimkaribisha Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mkurugenzi wa Serikali za Mitaa Ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt. Charles Mhina amesema Ofisi ya Rais TAMISEMI ilianzisha vituo vya biashara na Uwekezaji ili kuondoa adha kwa wajasiriamali ambapo watoa huduma wote wapo na walibaki ni Maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania ambapo sasa vifaa hivyo kwa ajili ya hao vimepatikana.

Pamoja na kutoa huduma za biashara na leseni huduma nyingine ni kutoa elimu ya mlipa kodi, kuandaa takwimu zinazohusiana na biashara na uwekezaji  kama vile masoko, bidhaa zinazozalishwa, biashara zilizopo na maeneo ya uwekezaji.

Vituo hivyo vya biashara vitakuwa na wataalam kutoka Halmashauri husika, Benki ya NMB, Mamlaka ya Mapato Tanzania, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Idara ya Uhamiaji kwa Halmashauri zilizopo pembezoni.    

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *