Afya

Serikali yasogeza huduma za afya karibu na wananchi

Dkt. Ntuli Kapologwe. (Picha na Maktaba ya OR-TAMISEMI)

Na . Angela Msimbira MTWARA

Mkurugenzi wa Idara ya afya, Ustawi wa Jamii na Lishe Dkt. Ntuli Kapologwe amesema kuwa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa imeweza kuhakikisha inasogeza huduma za afya karibu na wananchi kwa kujenga miundombinu bora ya afya, kuongeza wataalam na kuhakikisha kuna vifaa na vifaa tiba.

Akihojiwa leo kuhusu uzinduzi wa Kituo cha afya cha Mbonde kilichopo katika Halmashauri ya Mji wa Masasi Mkoani Mtwara kwa niaba ya vituo 352 vya kutolea huduma ya afya nchini Dkt. Ntuli Kapologwe amesema kazi ya OR-TAMISEMI ni kuratibu na kusimamia sera za afya nchini kuanzia ngazi wa Sekretarieti za Mikoa na Serikali za Mitaa.

Dkt. Kapologwe anafafanua kuwa uzinduzi huo unafanyika katika kituo cha afya Mbonde ikiwa moja ya vituo 352 vya kutolea huduma nchini ambavyo vimejengwa ndani ya miaka mitatu katika Serikali ya awamu ya Tano na kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi inayotaka uboreshaji wa huduma za afya nchini kwa kusogeza huduma hizo karibu na wananchi.

Ameendelea kusema Serikali imeamua kufanya maboresho ya vituo vya kutolea huduma nchini na kuhakikisha kuwa wananchi wanaweza kupata huduma za afya jirani na maeneo wanayoishi na huduma zinazotolewa kuwa zina ubora unaostahiki.

“ Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amekuwa akiweka msisistizo mkubwa katika Sekta ya Afya ikiwa ni maandalizi ya kuelekea kuwa nchi yenye uchumi wa kati ifikapo 2025hivyo ni vyema tukahakikisha kila mwananchi anakuwa na afya bora ili aweze kutekeleza majikumu yake kikamilifu katika jamii” Anafafanua Dkt. Kapologwe

Amesema kuwa maboresho hayo hayalengi katika suala zima la ujenzi wa miundombinu ya afya pekee bali yanaenda sambamba na kuongeza Rasilimali watu, upatikanaji wa dawa na vifa na vifaa tiba nchini.

Aidha Dkt. Kapologwe amesema katika vituo 352 vya kutolea huduma za afya nchini Serikali imeweza kukarabati Hospitali 6, ujenzi na ukarabati wa Zahanati 39 na vituo vya afya 304 nchini. Hii inaweka historia kubwa ambayo haijawahi kutokea tangu kupata kwa uhuru ambapo kulikuwa na na vituo 518.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *