Habari za mikoani

Serikali Yataka Halmashauri kubuni miradi ya Kimkakati

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji akionesha risiti ya EFD baada ya kununua chaki za Maswa mkoani Simiyu, baada ya kutembelea kiwanda cha chaki akiwa na Viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa na CCM wilaya ya Kondoa kwa lengo la kujifunza mkoa wa Simiyuunavyotekeleza sera ya viwanda.

Na Stella Kalinga, Simiyu

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji ametoa wito kwa Halamshauri zote nchini kubuni miradi ya kimkakati ya itakayoziongezea mapato badala ya kuendelea kutegemea ushuru na tozo mbalimbali kutoka kwa wananchi.

Dkt. Kijaji amayasema hayo wakati alipotembelea kiwanda cha kutengeneza chaki cha wilaya ya Maswa wakati wa ziara yake ya kujionea utekelezaji wa Sera ya Tanzania ya Vwanda Mkoani Simiyu akiwa na viongozi wa Halmashauri na Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Kondoa.

Amesema dhamira  ya Serikali ni kuhakikisha Halmashauri zote zinabuni miradi ya kimkakati ambayo itaziongezea mapato na akatoa wito kwa Halmashauri zote nchini kujifunza kwa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa ambayo imetengewa shilingi bilioni 8.2 na Serikali kwa ajili ya kutekeleza miradi miwili ya upanuzi wa Kiwanda cha Chaki na kujenga kiwanda cha vifungashio.

“Niwapongeze Simiyu mnafanya kazi nzuri, tunataka kuondoka kwenye ule ukawaida wa Halmashauri zetu kulalamika kuwa Serikali Kuu imechukua vyanzo vya mapato, Serikali Kuu haijachukua kinachohitajika ni ubunifu wa miradi kama Halmashauri ya Maswa ilivyofanya, nitoe wito kwa Halmashaui zote kubuni miradi, Serikali ipo tayari fedha zipo kwa ajili ya miradi ya kimkakati ya kuongeza mapato ya Halmashauri” alisema

 Mbunge wa Maswa Mashariki na Naibu Waziri wa Madini Mhe Stanslaus Nyongo ameiomba Serikali kutoa fedha hizo shilingi Bilioni 8.2 zilizotengwa kwa wakati ili Miradi iliyokusudiwa ya upanuzi wa kiwanda cha chaki na ujenzi wa kiwanda cha vifungashio iweze kutekelezwa kwa wakati.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Simiyu amesema katika kukiongezea kiwanda cha chaki uwezo wa  uzalishaji, Halmashauri ya Maswa imenunua eneo kwa ajili ya malighafi ya kutengenezea chaki katika Mkoa wa Singida.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa Dkt. Fredrick Sagamiko amesema Halmashauri hiyo imedhamiria kufikisha zaidi ya asilimia 75 ya mapato ya ndani yatakayotokana na viwanda vilivyopo na vinavyoendelea kujengwa wilayani humo.

Awali Dkt. Ashatu alitembelea eneo maalum lililotengwa kwa ajili ya uwekezaji katika viwanda la Halmashauri ya Wilaya ya Maswa mahali ambapo patajengwa kiwanda kikubwa cha kutengeneza chak(upanuzi wa hiki kilichopo) na kujenga kiwanda cha vifungashio

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji akisaini ubao kwa kutumia chaki za Maswa katika kiwanda cha chaki Maswa mkoani Simiyu, baada ya kutembelea kiwanda hicho akiwa na Viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa na CCM wilaya ya Kondoa kwa lengo la kujifunza mkoa wa Simiyu unavyotekeleza sera ya viwanda

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *