Elimu

Serikali Yataka Wadau Kuwa na Mtazamo Chanya katika Sekta ya ELimu

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala Mikoa na Serikali za Mitaa (OR – TAMISEMI) Selemani Jafo akitoa hotuba ya kufunga Mkutawano wa Pamoja wa Mwaka wa Wadau wa Elimu Jijini Dodoma ambapo amewataka Wadau kuendelea Kushirikiana na Serikali Kuboresha Elimu 
Baadhi ya Washiriki wa Mkutano wa Pamoja wa Mwaka wa Wadau wa Elimu uliofanyika Jijini Dodoma wakifuatilia kwa makini hotuba ya Mgeni Rasmi Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,  TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo (Hayupo pichani)

 

Na. Fred Kibano na Magdalena Dyauli

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala Mikoa na Serikali za Mitaa (OR – TAMISEMI) Selemani Jafo amewaasa Wadau wa elimu kufungua minyororo ya kifikra kwa kujadili na kutathmini kwa upana mustakabali wa elimu nchini kwa maendeleo ya Taifa.

Jafo ameyasema hayo leo alipokuwa akifunga Mkutano wa Pamoja wa Mwaka wa Wadau wa Elimu Jijini Dodoma na kusisitiza kuwa lazima Asasi na Mashirika binafsi yanayoshughulikia elimu yashirikiane na Halmashauri ili kupata takwimu sahihi za masuala ya elimu.

“mashirika haya yaweke mipango ya kushirikiana na Halmashauri katika masuala ya elimu, lakini sio kila wanalosema Wadau liwe baya tu, yapo pia masuala mazuri ya kuongelea” alisema waziri ajafo.

Waziri Jafo pia amewaagiza Maofisa Elimu wa Mikoa na ngazi zote wafanye kazi kwa bidii kwa sababu wao ndio watekelezaji hasa wa mikakati inayowekwa na Wadau wa Elimu.

“Maafisa Elimu mnaposhindwa kutekeleza wajibu wenu hata mipango inayopangwa inaharibika, ndani ya mpango huu wa mwaka mmoja Afisa Elimu inakubidi ujitathmni umefanya nini kubadilisha mwenendo wako”

Aliwashukuru Wadau wote kwa kufanya tathmini na kujadiliana kwani malengo mengi ya elimu hayatoweza kufikiwa katika kuelekea Tanzania ya Viwanda kama tathmini haitafanyika.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Dkt. Anne Maria Semakafu amesema tathmini waliyoifanya kwa siku nne kuhusu Sekta ya Elimu kumeimarisha uibuaji wa masuala mbalimbali kama vile Elimu Ndani na Nje ya Mfumo Rasmi na Elimu ya Ufundi Stadi ambapo maazimio yote yatafikishwa Serikalini.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Mtandao wa Elimu Nchini (TENMET) Lidya Wilbard, aliishukuru Serikali  kwa kuwapa Wadau wa Elimu nafasi ya kutathmini na kujadiliana mustakabali wa elimu nchini na kuiomba Serikali itoe ufafanuzi zaidi kuhusu Sera ya Elimu Bure ili kuondoa mkangnyiko wa mawazo juu ya sera hiyo miongoni mwa Wadau nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *