Habari za Kiuchumi/Kilimo

Serikali Yatoa Wito Kwa Benki ya DCB Kuwainua Wajasiriamali

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mhe. Selemani Jafo (katikati) akiwa na Godfrey Ndalahwa Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Kibiashara ya DCB Tanzania na Bi. Rahma Ngassa Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mawasiliano DCB Dodoma na kushoto ni Joseph Njile Meneja wa Tawi la Benki ya DCB Dodoma. Waziri Jafo ametoa wito kwa Benki hiyo kuwajengea uwezo wa kijasiriamali wateja wake ili wapate matokeo chanya kwa uchumi wao na nchi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe. Selemani Jafo akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watumishi wa Benki ya Biashara ya DCB Tawi la Dodoma alipotembelea Benki hiyo leo jijini Dodoma.

Na. Fred Kibano na Majid Abdulkarim

Benki ya Biashara ya DCB iliyoka chini ya, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), imetakiwa kuwajengea uwezo mzuri wateja wao katika kufanyikisha mahitaji yao ya ujasiriamali ili kuweza kupata matokeo chanya na kupata kipato kizuri kitakacho wasaidia kuinua uchumi wa Nchi.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe. Selemani Jafo wakati alipotembelea Benki ya Biashara ya DCB tawi la Dodoma leo jijini Dodoma.

Mhe.Jafo ameutaka uongozi wa Benki ya DCB kuwapatia elimu wateja wao juu ya kufanya ujasiriamali au biashara zao kwa kuwaongoza namna gani wataweza kufikia malengo yao katika shughuli wanazo fanya ili kuhakikisha wanafikia malengo yao kwa ufasaha.

Aidha, Jafo amesema kwa sasa ni wakati wa Benki ya DCB kujenga ushirikiano mzuri na Uongozi wa Jiji la Dodoma na wao kwa kuwa na hisa katika benki hiyo kwani Jiji la Dodoma ni miongoni mwa majiji kumi yanayofanya vyema katika ukusanyaji wa mapato hapa nchini .

“Natoa wito kwenu kuwa mnatakiwa kuwa na ukarimu kwa wateja wenu ili kuweza kupata matokeo mazuri zaidi ya haya, kwani lugha nzuri utakayo tumia katika kumuhudumia mteja wako ndo itakayo mfanya mteja kufurahia huduma yako na kupata wateja wengi zaidi ya hawa mlonao kwa sasa”Ameongezea Mhe. Jafo.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Biashara ya DCB Bw. Godfrey Ndalahwa amesema kuwa mpaka sasa uboreshaji wa huduma na mahusiano ya wateja  umekuwa ndio chachu ya kumwezesha mteja kufungua  akaunti na kufanya miamala yote ya kibenki, kutunza fedha na kuwekeza  kwa kutumia simu yake ya mkononi.

Bw. Ndalahwa ameongezea kuwa benki ina malengo ya kujitanua zaidi tofauti na hapo awali ilipokuwa benki ya Jumuiya ya Wananchi wa Dar es salaam (Dar es Salaam Community Bank) na kwa sasa malengo ni kujitanua katika halmashauri, manispaa na majiji nchini.

“Benki hii ilianzishwa mnamo mwaka 2001 ikiwa kama benki ya wananchi wa Dar es salaam, Rais wa Awamu ya Tatu, mnamo mwaka 2001, alitoa agizo la kuanzisha benki hii na ikiwa kama benki ya Jumuiya ya Wanachi kupitia Manispaa za Jiji la Dar es salaam ikiwemo Halmashauri ya Jiji la Dar ves Salaam” Amehitimisha Bw. Ndalahwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *