Elimu

Serikali yawataka Maafisa Elimu wa Mikoa na Wilaya kuleta mageuzi ya elimu

Na Mathew Kwembe

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI, Mhandisi Mussa Iyombe amesema pamoja na juhudi ambazo serikali inafanya, sekta ya elimu imeshindwa kuleta mageuzi ambayo serikali na wananchi wanayategemea.

Mhandisi Iyombe aliyasema hayo jana  kwenye kikao kazi maalumu kwa watendaji wa elimu katika ngazi ya taifa, mikoa na halmashauri kinachofanyika kwa siku mbili jijini Dodoma.

“Mwaka 2015 watanzania walipiga kura kwa kutaka mabadiliko, mpaka sasa sekta ya elimu hakuna mabadiliko yaliyofikiwa tofauti na sekta ya afya, bado akili zenu zimelala pale pale,” alisema.

Aliongeza: “Watumishi wasiotaka mabadiliko waondoke wenyewe na kama hawataki kuondoka tutawaondoa hatuwezi kulazimisha mtu kufanya kazi kimazoea na ndiyo maana wengine wanataka kuhonga ili wapate nafasi badala ya kufanya kazi sawasawa.”

Alisema anachukuziwa na kuona mambo hayaendi vizuri kwenye sekta ya elimu wakati maofisa wa elimu ngazi ya mikoa, wilaya na kata wapo na kuonya kuwa endapo kuna kiongozi anaona haweza kuwa chachu wa mabadiliko katika eneo lake basi kiongozi huyo hatoshi.

“ Kuna mambo mengi mabaya yanatokea katika sekta ya elimu lakini viongozi nyinyi mpo tu na hakuna hatua yeyote mnayochukua huku mkisubiri maamuzi kutoka makao makuu.”

Mhandisi Iyombe alitolea mfano tukio la kuchapwa viboko hadi kufa kwa kwa mwanafunzi wa shule ya msingi Kibeta katika Manispaa ya Bukoba ambapo taarifa hiyo aliipata kutoka kwa mdhibiti wa ubora wa elimu wakati maafisa elimu mkoa, wilaya, kata wapo.

“Hakuna tukio baya na la kinyama kama lililofanywa na mwalimu wa shule ya Msingi Kibeta wilayani Bukoba lakini hakuna ripoti zozote zilizotolewa na wahusika na badala yake taarifa ilitolewa na Ofisa Uhakiki Ubora, wakati mwalimu mkuu yupo, afisa elimu kata, wilaya na mkoa wapo na unapowauliza wanasema eti ni tukio kubwa litaonekana kwenye vyombo vya habari yaani Mimi katibu mkuu nifanye kazi na kupeleka taarifa kwa Mheshimiwa Rais kupitia vyombo vya habari wakati uongozi upo kweli nyie mnatosha?” alihoji Mhandisi Iyombe

Alisema kutowajibika ipasavyo kwa viongozi hao kumechangia hata tabia ya uvujaji na uwizi wa mitihani unaofanywa na baadhi ya shule kwa lengo la kujipatia umaarufu, lakini hakuna hatua zozote zinazochukuliwa.

Aidha, Katibu Mkuu amewataka viongozi hao ambao kwa nyadhifa zao wanaingia kwenye vikao vya maamuzi kuhakikisha wanajenga hoja za nguvu ili halmashauri zitenge fedha kwa ajili ya miundombinu ya shule katika eneo husika.

“ Mnapata nafasi ya kuingia kwenye vikao vya halmashauri, msiende huko kusinzia, mwende mkajenge hoja ili halmashauri zitenge fedha za ndani kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya shule maana wewe ndio unajua hali ya shule zako,”

Aliongeza: “ Kataeni kuwa na shule za nyasi, watoto wanakaa chini wakati kuna fedha za ndani za halmashauri zipo na kuna maeneo halmashauri zina mapato mengi ya ndani.”

 

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *