Habari za Kiuchumi/Kilimo

Serikali yaziagiza Halmashauri Kutumia Mashine katika Kukusanya Mapato

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI (ELIMU) Tixon Nzunda akikagua mojawapo ya Mradi wa kikundi cha wakulkima wadogo cha Big Power Star wilayani Kibondo, kulia ni mmoja wa wanakikundi hicho Bwana Salu Ndalu
Mwananchi mjasiriamali akianika dakaa katika kichanja cha kuanikia dagaa kandokando ya ziwa Tanganyika Manispaa ya Kigoma, mkoani Kigoma

Na Fred Kibano

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa – Ofisi ya Rais TAMISEMI (ELIMU) Tixon Nzunda, ameziagiza halmashauri za mkoa wa Kigoma kutumia mashine za kukusanya mapato na kutumia vituo vya biashara badala ya kusubiri uzinduzi rasmi.

Nzunda ametoa kauli hiyo wakati wa ziara yake katika halmashauri za wilaya Kigoma Ujiji, Kigoma Manispaa, Buhigwe, Kasulu Mji, Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Kasulu Mji na Halmashauri ya wilaya ya Kibondo ambapo amewataka Watendaji kuanza kutumika kwa vituo vya biashara vilivyojengwa kwa ushirikiano wa Serikali na Mradi wa Kuboresha Mazingira ya Biashara (LIC) ambavyo vimekamilika bila kusubiri uzinduzi uliopangwa

Pia amewataka Watendaji wa Halmashauri hizo kuhakikisha maandiko yote ya miradi ya kuboresha mazingira ya biashara (LIC) yawe yamekamilika kabla ya tarehe 12 Desemba, 2018 na kuwasilishwa Serikalini na Wadau kwa ajili ya kupatiwa fedha za kuendeshea miradi hiyo ambayo fedha zake zipo.

“andikeni BOQ za miradi kabla ya tarehe 12 Desemaba, miradi yote ikamilke na kuwasilishwa LIC, sio msubiri fedha hizi zirudi Denmark, Katibu Tawala na Wakurugenzi nasema Wakuu wa Idara wanaoshindwa kuandikia miradi hii wachukuliwe hatua mara moja” alisema Nzunda.

Nzunda ameipongeza Halmashauri ya wilaya ya Kibondo kwa kufanya vizuri katika miradi yao ambayo ni ya kimkakati kama ofisi ya kituo cha biashara, viwanda viwili vya kuchakata zao la muhogo, mradi wa umwagiliaji Nyendera na kituo cha kufundishia kazi za ujasiriamali.

Naye Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya wilaya Buhigwe Anosta Nyamoga, amesema mradi wa Kuboresha mazingira ya biashara umesaidia kuimarisha miundombinu ya mifumo ya mapato pamoja na utoaji wa mashine za kukusanyia mapato (Pos) ambazo zimeongeza mapato maradufu.

“kabla ya matumizi ya Pos 2015/2016 halmashauri ilikusanya 262,313,284 lakini baada ya matumizi ya Pos mwaka 2017/2018 halmashauri ilikusanya kiasi cha shilingi 371,224,164 ongezeko ambalo halikuwepo awali”

Mradi wa Kuboresha Mazingira ya Biashara (Locasal Investment Climate) unafanywa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Denmark chini ya Shirika lake la Maendeleo DANIDA kwa lengo la kuboresha huduma za kibiashara na mazingira yake kwa kuwajengea uwezo wananchi ili kuondoa vikwazo zinavyochangia kutokukuwa kwa biashara na uchumi katika halmashuri zote za mikoa ya Dodoma na Kigoma kwenye.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *