Video

Sijaridhika na Ujenzi wa Hospitali ya Wilaya Chamwino – Jafo

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo pamoja na uongozi wa mkoa wa Dodoma na Wilaya ya Chamwino akiangalia ukubwa wa zege la msingi kwa kutumia ‘tape’ na unyoofu wa zege la msingi kwa kutumia pima maji huku fundi akiweka vipimo hivyo alipofanya ziara ya kujionea ujenzi wa hospitali ya wilaya.

Na Fred Kibano

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Selemani Jafo ameutaka Uongozi wa Kamati ya ujenzi wa Wilaya ya Chamwino kuongeza spidi ya ujenzi wa Hospitali mpya ya Wilaya.

Hayo ameyasema leo katika ziara yake ya kukagua ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Chamwino inayojengwa katika kijiji cha Mlowa barabarani kilichopo wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma.

Jafo amesema kuwa hajaridhishwa na spidi ya ujenzi wa hospitali hiyo na kuwataka uongozi pamoja na Mkandarasi kuongeza kasi ili kukamilisha kwa wakati uliowekwa.

“Sijaridhishwa na spidi ya ujenzi wa hospitali hii,naomba muongeze spindi,fanyeni haraka muagize vifaa vya ujenzi ili kukamilisha kwa wakati tulioweka”amesema Jafo

Hata hivyo amesema kuwa fedha za ujenzi wa hospitali hiyo na nyingine zimetolewa na Serikali inayoongozwa na Rais John Magufuli ili kuweza kuwahudumia wananchi wake.

“Vilevile wakandarasi wanaotekeleza ujenzi wa hospitali hii mnatakiwa kujenga majengo yote kwa wakati na kulingana na thamani ya fedha zilizotolewa na Serikali”amesisitiza Jafo.

Aidha, amewashukuru wananchi wa Kijiji cha Mlowa barabarani  kwa kukubali kutoa ardhi  ya  eneo lenye ukubwa wa ekari 24  kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Chamwino Vumilia Nyamoga amesema kuwa ujenzi wa miundombinu ya hospitali hiyo ulianza rasmi januari 22, 2019 na mradi unatarajiwa kutumia   gharama ya sh bilioni 1.5 zilizotolewa na Serikali.

Mradi wa ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Chamwino umeshirikisha wananchi wa Kijiji cha Mlowa barabarani na lilikuwa ni pendekezo la Mhe Mbunge wa Mtera Job Lusinde baada ya kupata hospitali ya Uhuru ambayo pia itajengwa wilayani Chamwino

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *