Afya

Simamieni Vema Rasilimali Fedha – Dkt. Chaula

 

Naibu Katibu Mkuu (Afya) Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Dkt. Zainab Chaula akizungumza na Wasaidizi wa Hesabu (hawapo pichani) wakati wa kufunga Mafunzo ya FFARS yaliyoratibiwa na OR-TAMISEMI jana jijini Dodoma
Baadhi ya Wasaidizi wa Hesabu wanaofanya kazi katika Vituo vya Afya pamoja na Hospitali mikoa yote nchini wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu (Afya) OR-TAMISEMI, Dkt. Zainab Chaula (hayupo pichani) akizungumza nao wakati wa kufunga Mafunzo ya FFARS yaliyoratibiwa na OR-TAMISEMI jana jijini Dodoma

Na Ainess Makassi

Wasaidizi wa hesabu wanaofanya kazi katika Vituo vya Afya pamoja na Hospitali za mikoa yote nchini wameaswa kulinda na kusimamia vizuri rasilimali fedha ili ziweze kutumika kunufaisha jamii kama ilivyokusudiwa na Serikali.

Hayo yalisemwa jana na Naibu Katibu Mkuu (AFYA) Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Dkt. Zainab Chaula wakati wa kufunga mafunzo ya ‘Facility Financial Accounts Report System’ (FFARS) kwa wahasibu wasaidizi waliohudhuria mafunzo hayo yaliyofanyika kwa muda wa siku mbili jijini Dodoma.

Dkt. Chaula alitoa maelekezo kuwa hatamtoa Mhasibu yeyote katika nafasi yake kwa kuwa OR – TAMISEMI ndio mratibu wao hivyo wote watapewa mikataba ya miaka miwili huku akiwahimiza kufanya kazi kwa bidii na umoja.

“Kwa kuwa mpo kazini na mnajituma, tutawachukua nyote na tutatoa mikataba ya miaka miwili, msikubali mtu aibe, tulisema hapa kazi ni kazi tu! Lazima tumsaidie Mheshimiwa Rais kuibadilisha hii nchi na tumshukuru Mungu kwa baraka aliyotupatia” alisema Dkt. Chaula.

Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Dkt. Anna Nswilla amewapongeza washiriki hao kwa kufanya kazi nzuri na kuwahimizia kuzidi kujituma kazini.

“Ninyi ni sehemu ya Afya na maboresho pamoja na kutoa huduma bora kwa wagonjwa, mkikaa bila kufanya kazi ama kumnyanyapaa mgonjwa hakuna malipo, hivyo ni busara kuendelea kujituma na kuzingatia maadili kama mafunzo haya yalivyohimiza” alisema Dkt. Nswilla.

Kwa upande wake Mkurugenzi Huduma za Kinga Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Leonard Subi aliwasisitizia wasaidizi hao wa hesabu kuzingatia uadilifu na usimamizi mzuri wa rasilimali fedha ili kuonyesha umuhimu wa ujuzi walioupata katika mafunzo ya FFARS kama ambavyo imekusudiwa.

“Rasilimali fedha inatakiwa itumike vizuri katika maeneo yetu ya kazi ili kuboresha huduma za afya kwa jamii na kupunguza vifo” Alisema Dkt. Subi.

Mhasibu Msaidizi Kituo cha Afya Tingi kilichopo mkoani Lindi, Khatiba Gonza ameahidi kuwa wasimamizi mzuri wa rasilimali fedha pamoja na kushiriki kikamilifu katika utoaji wa huduma za afya ili kuboresha huduma hizo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *