Habari za mikoani

Simiyu kupata Shule ya Vipaji Maalum, Kuchagiza Viwanda Mkoani humo

Baadhi ya wananchi wa Kata ya Malambo Mjini Bariadi wakichimba msingi wa wa ujenzi wa madarasa zaidi 40 na mabweni 15 ya Shule ya Sekondari Simiyu ambayo inatarajiwa kuwa shule ya vipaji maalum ya mkoa wa Simiyu.

Na Stella Kalinga, Simiyu

Wananchi wa Wilaya ya  Bariadi Mkoani Simiyu  kwa kushirikiana na Mkuu wa Wilaya hiyo Festo Kiswaga  wamejitokeza kwa wingi  kuchangia nguvu kazi , kuchimba msingi wa ujenzi wa madarasa zaidi 40 na mabweni 15 ya Shule ya Sekondari Simiyu

Wananchi hao wamejitokeza kwa wingi katika shule ya sekondari ya Simiyu kwa lengo la kuunga jitihada za Mkuu wa Mkoa wao Anthony Mtaka za kuhakikisha wanakuza na kurudisha heshima ya elimu Mkoani humo.

Wamesema  kuwa wameguswa na uamuzi wa Serikali wa kuona  umuhimu wa kuboresha mazingira rafiki ya kujifunzia wanafunzi na kujenga shule kubwa ya vipaji maalum ambayo itakuwa ni msaada na utambulisho wa  Mkoa wao hasa wakati huu ambapo serikali imejizatiti katika mapinduzi ya viwanda.

Yohana Musa mkazi wa mji wa Bariadi amesema kuwa wameguswa sana na uamuzi wa Serikali ya Mkoa ikiongozwa na Mkuu wao wa Mkoa Anthony Mtaka wa kuwekeza katika elimu ambayo itawasaidia watoto wao kufikia malengo waliyojiwekea.

“chini ya uongozi wa Mkuu wa Mkoa  pamoja na Mkuu wa Wilaya, Mkoa wetu utakuwa na shule bora itakayochukua idadi kubwa ya wanafunzi walio na vipaji maalum ndani na nje ya Mkoa wa Simiyu, alisema Musa.

Mwenyekiti wa mtaa wa mnara wa voda Songera Magenda amesema kuwa wananchi wake wamekuwa na muamko wa kushiriki katika shughuli za kimaendeleo ili kujenga Mkoa wao.

Magenda amesema kuwa kupitia nguvu kazi za wananchi wake ,ni matumaini yake kuwa ujenzi wa shule hiyo utaenda kwa kasi na kukamilika mapema mwaka huu ambapo ukikamilika utatoa fursa kwa wanafunzi wenye vipaji maalum wa Mkoa wa Simiyu kusoma hapo.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Festo Kiswaga  amesema endapo shule hiyo ikikamilika itakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi zaidi ya 1000 kwani inatarajiwa kuwa na mabweni 10 pamoja na vyumba vya madarasa visivyopungua 40.

Kiswaga amesema kuwa shule hiyo imeanza kujenga kwa jitihata za uongozi wa Mkoa ambao lengo kuu ni kuona Mkoa wa Simiyu nao unakuwa na shule kubwa,nzuri ya wanafunzi wa vipaji maalum kama ilivyo mikoa mingine.

Kiswaga pia ametoa wito kwa wanasimiyu wote wenye mapenzi mema na elimu ,waone umuhimu wa kujitolea na kuchangia ujenzi wa shule hiyo ili iweze kukamilika kwa wakati na kusaidia kundi kubwa na wanafunzi kusoma shuleni hapo.

Mkoa wa Simiyu ni moja ya Mikoa inayofanya vizuri kutokana na mshikamano uliopo baina ya vongozi na wananchi kutokana na sense ya watu na makaazi ya mwaka 2012, mkoani Simiyu kuna jumla ya watu  1, 584,157.

Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Mhe.Festo Kiswaga (mwenye koleo) akishirikiana na wananchi kwa Kata ya Malambo mjini Bariadi kuchimba msingi wa ujenzi wa madarasa zaidi 40 na mabweni 15 ya Shule ya Sekondari Simiyu ambayo inatarajiwa kuwa shule ya vipaji maalum ya mkoa wa Simiyu.
Katibu wa CCM Wilaya ya Bariadi, Ndg.Nicholuos Kasendamila akishirikiana na wananchi kwa Kata ya Malambo mjini Bariadi kuchimba msingi wa ujenzi wa madarasa zaidi 40 na mabweni 15 ya Shule yaSekondari Simiyu ambayo inatarajiwa kuwa shule ya vipaji maalum ya mkoa wa Simiyu..

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *