Habari za mikoani

Simiyu Yapokea vitabu 174, 188 vya Darasa la Nne

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Msingi Somanda A, mara baada ya makabidhiano ya vitabu vya Darasa la nne mkoani humo na Mwakilishi wa Taasisi ya Elimu Tanzania(TET) Bw. Didas Hamsini, yaliyofanyika Julai 05, 2018 katika Viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mjini Bariadi.

Na Stella Kalinga, Simiyu

Mkoa wa Simiyu umepokea jumla ya vitabu 174,188 awamu ya kwanza kwa masomo ya Kiingereza na Hisabati, vyenye thamani ya takribani  shilingi milioni 348 kwa ajili ya wanafunzi wa darasa la nne, ambavyo ni sawa na uwiano wa mwanafunzi mmoja kwa kitabu kimoja.

Akizungumza na viongozi, baadhi ya walimu na wanafunzi wa mkoa wa Simiyu kabla ya kukabidhi vitabu hivyo kwa Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Anthony Mtaka Julai 05 mwaka huu mjini Bariadi, Mwakilishi wa Taasisi ya Elimu Tanzania(TET) Bw. Didas Hamsini, amesema Taasisi hiyo imejipanga kuhakikisha vifaa vyote vya kielimu ikiwemo vitabu, vifaa vya maabara na vifaa vingine vinavyohitajika  vinapatikana.

Amesema utoaji wa vitabu 29,003 kwa kila somo kwa wanafunzi wa darasa la nne Mkoani Simiyu ni sehemu ya utekelezaji wa elimu bila malipo, huku akibainisha kuwa Taasisi ya Elimu inatarajia kuzalisha vitabu 681, 527 kwa ajili ya wanafunzi wa darasa la nne nchi nzima.

Afisa Elimu Mkoa wa Simiyu, Mwl. Julius Nestory alisema wamepokea vitabu awamu ya kwanza kwa masomo ya kiingereza na hisabati kwa uwiano wa kitabu kimoja mwanafunzi mmoja, huku akibainisha kuwa vitabu salia vinatarajiwa kuwasilishwa mkoani humo kuanzia tarehe 16 Julai, 2018 huku  akiwataka walimu na wanafunzi kuvitumia vitabu hivyo kama ilivyokusudiwa.

“Naishukuru sana Serikali kwa kutoa vitabu hivi hadi sasa tuna wanafunzi  53, 187 darasa wa nne na vitabu tulivyopokea kwa awamu hii kwa masomo ya Hisabati na Kiingereza, kila mwanafunzi wa Mkoa wa Simiyu atapata kitabu cha kwake, kwa masomo manne yanayobaki tumeahidiwa kuwa baada ya majuma mawili vitakuwa vimefika” alisema Afisa Elimu Mkoa.

Kwa upande wao wanafunzi wa mkoa wa Simiyu wameishukuru Serikali kwa kuwaletea vitabu, hivyo ambavyo wanaamini vitawasaidia kujisomea na kuinua ufaulu hatimaye kuufikisha mkoa huo katika mikoa kumi bora inayofanya vizuri kitaaluma.

“Tunaishukuru sana Serikali kwa kuwaleta hivi vitabu, tunaamini vitawasaidia wadogo zetu wa darasa la nne kujifunza na kuongeza ufaulu na siku moja mkoa wetu na sisi utakuwa kati ya mikoa bora inayofanya vizuri kitaaluma “ alisema Liku Malisha mwanafunzi wa darasa la saba Shule ya Msingi Somanda A.

Kwa upande wake Mbunge wa Itilima Mhe. Njalu Silanga ameishukuru Serikali kwa kutoa vitabu hivyo na akatoa wito kwa walimu na wanafunzi mkoani humo kuhakikisha kuwa vitabu hivyo vinawezesha kuongeza ufaulu kwa kuwa mkoa huo umeshajipanga kutokomeza ujinga na kuwa mkoa kiongozi katika suala la  elimu.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka ameipongeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kutimiza ahadi yake na kujibu kilio cha muda mrefu cha wazazi, walimu na wanafunzi juu ya changamoto ya ukosefu wa vitabu wa darasa la nne.

Ameongeza kuwa vitabu hivyo vitausaidia mkoa wa Simiyu kufikia malengo yake katika kuongeza ufaulu na kuboresha  Sekta ya Elimu, ambapo amebainisha kuwa kupata vitabu hivyo, kupata walimu, kukamilisha miundombinu na mwamko wa wazazi kuchangia chakula watoto wao shuleni kutaufanya mkoa huo kushindana kielimu katika miaka ya mbeleni.

Katika hatua nyingine Mhe. Mtaka amewataka walimu mkoani humo kuwafundisha kwa moyo, wanafunzi kuvitumia vema vitabu hivyo  na wazazi kuwafuatilia watoto wao katika masomo ili wanafunzi waweze kufanya vizuri, kwa kuwa ufaulu wa mwanafunzi hutegemea  ushirikiano kati ya walimu, wanafunzi na wazazi.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Antony Mtaka mara baada yakufanya makabidhiano akitioa maelezo juu ya matumizi ya sahihi ya vitabu hivyo
Mwakilishi wa Taasisi ya Elimu Tanzania(TET) Bw. Didas Hamsini(kulia) akimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akiwa na baadhi ya viongozi na wanafunzi wa Shule ya Msingi Somanda A vitabu vya Darasa la nne mkoani humo, makabidhiano hayo yalifanyika Julai 05, 2018 katika Viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mjini Bariadi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *