Mafunzo

TAMISEMI, PS3 na TSC Kuboresha OPRAS ya Walimu kwa Matokeo

 

Na. Fred Kibano

Mkurugenzi wa Serikali za Mitaa Ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt. Charles Mhina, amefungua mafunzo ya kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa OPRAS kwa ajili ya walimu wanaofundisha darasani kwa wawezeshaji wa Kitaifa Jijini Dodoma na kuwataka washiriki kuleta matokeo chanya katika sekta ya Umma nchini.

Mkurugenzi wa Serikali za Mitaa Ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt.Charles Mhina akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo ya mafunzo ya kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa OPRAS kwa ajili ya walimu wanaofundisha darasani kwa wawezeshaji wa Kitaifa Jijini Dodoma

Akifungua mafunzo hayo katika ukumbi wa African Dreams Hotel Jijini Dodoma, Dkt. Mhina amewataka washiriki kutumia nafasi hiyo adimu ya mafunzo ili kuleta mabadiliko ya mfumo mzima wa upimaji wa utendaji katika sekta ya umma ujulikanao kama OPRAS. Dkt Mhina alibainisha kuwa katika sekta ya Umma, sekta ya Elimu ndiyo inachukua asilimia kubwa ya watumishi wa Serikali hapa nchini na hii imepelekea kuanza maboresho katika sekta ya elimu.

“tumiemi nafasi hii mkalete mabadiliko katika upimaji wa utendaji kwani hakuna kundi la Utumishi wa Umma lisilotekeleza mfumo wa OPRAS, watumishi wote lazima wajaze, hivyo kundi hili la wawezeshaji wa kitaifa ndilo linalotegemewa katika kufundisha wengine katika sekta ya Elimu”.

Dkt. Mhina amesema watumishi wote wa Umma wanapaswa kufanya kazi kwa bidii ili kuleta matokeo, na hii ndiyo sababu ya kumpima mfanyakazi. “Kila mtumishi anapaswa afanye kazi kwa bidii na kuleta matokeo, sisi kama wataalam tunapaswa kutambua na kujua eneo hili muhimu la OPRAS na ndio maana kuna maboresho katika eneo hili”

Dkt Mhina alibainisha kuwa Mfumo huu umeanza kutekelezwa Mwaka 2004 na alitaja changamoto za utekelezaji wa mfumo wa OPRAS ambazo zinaweza kutatuliwa kwa watekelezaji kupata uelewa juu ya mfumo. Dkt Mhina ameshukuru Shirika la Misaada la Marekani (USAID) kupitia Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta ya Umma ‘PS3’ kwa kugharamia mafunzo ya timu ya wawezeshaji wa kitaifa wa sekta ya elimu.

Kwa upande mwingine, Dkt. Josephine Kimaro ambaye ni Msimamizi wa Kitengo cha Mifumo ya Rasilimali Watu (HR Team Lead) kutoka PS3 amesema lengo la mafunzo hayo ni kuboresha utekelezaji wa mfumo wa OPRAS kwa Walimu wanaofundisha darasani. Dkt Kimaro alibainisha kwamba mnamo Februari 2017, OR-TAMISEMI, OR-Utumishi, Tume ya Utumishi wa Umma na Mradi wa PS3 walishirikiana katika utafiti wa kubaini changamoto za utekelezaji wa mfumo wa OPRAS katika Mamlaka za Serikali za Mitaa. Utafiti huu uligundua changamoto ya ujazaji wa malengo ya OPRAS na kupelekea makubaliano ya kuanza kutatua changamoto hii kwa kurahisisha ujazaji wa malengo ya OPRAS kwa Walimu wa darasani.

Aidha, Dkt. Kimaro ameishukuru Serikali kwa kuwa mshirika mkubwa katika uimarishaji wa mifumo mbalimbali, ikiwemo ya Rasilimali Watu katika Utumishi wa Umma. PS3 imefanya kazi na Mamlaka za Serikali Mitaa katika kuboresha upangaji wa Rasilimali Watu kwa kuzingatia uzito wa kazi na vipaumbele vya halmashauri, pia katika kutengeneza mipango ya motisha kwa watumishi ambapo kuna Halmashauri zinatenga bajeti kwa ajili ya motisha, na nyingine zimeanza utekelezaji wa mipango hiyo. Aidha, Mradi umetekeleza uboreshaji wa masjala za Halmashauri 30 hapa nchini kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika sekta ya umma.

Naye Bi. Neema Lemunge ambaye ni Mwakilishi wa Katibu Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) amewashukuru Programu ya PS3 kwa kuendelea kufadhili baadhi ya miradi na mifumo ambayo inaleta manufaa nchini hususani katika Mamlaka za Serikali za Mitaa. 

Mafunzo hayo ya siku nne yanafadhiliwa na Mradi wa Uimarishaji Mifumo ya Sekta ya Umma ‘PS3’ kwa ushirikiano wa pamoja na Ofisi ya Rais-TAMISEMI na Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC).

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *