Video

TAMISEMI yaandaa mwongozo mpya wa usimamizi wa mapato kwa Halmashauri

Na Mathew Kwembe

Serikali imesema kuwa mwongozo mpya wa ukusanyaji mapato katika halmashauri unalenga kuongeza wigo wa makusanyo ya mapato kwa kuwatoza watu wengi badala ya wachache na hivyo kuziwezesha halmashauri kukusanya mapato mengi zaidi.

Kauli hiyo imetolewa jana na Mratibu wa Mradi wa kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Bi Beatrice Njawa mara baada ya ufunguzi wa kikao cha kujadili Mwongozo wa Usimamizi Ukusanyaji Mapato katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi ndogo ya TAMISEMI iliyopo jijini Dar es salaam.

Alieleza kuwa mwongozo wa usimamizi wa mapato utapanua wigo kwa kuwatoza wale wote wanaostahili kutozwa mapato mbalimbali ikiwa ni pamoja na ushuru na kodi mbalimbali za Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Bi Njawa aliongeza kuwa mwongozo mpya sambamba na kuongeza wigo wa ukusanyaji mapato ya halmashauri umezingatia kushirikisha maoni ya wadau hususani sekta binafsi ili waweze kutoa elimu kwa wadau wao wa namna bora ya kuutekeleza mwongozo huo ili kufikisha malengo yaliyokusudiwa.

“Kupitia mwongozo huu tumeshirikisha sekta binafsi ambao watatusaidia kutambua baadhi ya ya shughuli za kiuchumi zilizopo katika maeneo yao ili tuweze kuibua vyanzo vipya isipokuwa kwa tahadhali kwamba havitakuwa kero katika jamii ya wafanya biashara.

Mapema akifungua kikao hicho kwa niaba ya Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es salaam bwana Abubakar Mussa Kunenge alisema kuwa Mwongozo huo ni jitihada za Serikali za kuziwezesha Halmashauri kukusanya Mapato ya Vyanzo vya Ndani kwa ufanisi na kikamilifu. Kadhalika, kuweka mikakati ya kuwezesha kuwepo kwa mazingira wezeshi ya kufanya biashara na uwekezaji.

Aliongeza kuwa mwongozo huo unalenga kuweka utaratibu rahisi wa utambuzi wa Fursa za kiuchumi na Sekta ya uzalishaji, utambuzi wa Walipa kodi, taarifa na takwimu za kodi, namna ya kusimamia na kukusanya mapato, ushirikishwaji wa wadau mbalimbali katika mipango na utekelezaji wa mikakati ya ukusanyaji mapato, kuongeza uwajibikaji na uwazi katika kukusanya na kutumia mapato yaliyokusanywa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi kutoka Idara ya Serikali za Mitaa Ofisi ya Rais TAMISEMI Bwana Shomari Mukhandi alisema kuwa Ofisi yake imeona ni vyema kukaa na wadau kujadili rasimu ya mwongozo huo ili kupata maoni ya kila mshiriki ili kuboresha Mwongozo wa Ukusanyaji Mapato kulingana na mahitaji ya Sekta mbalimbali za Kiuchumi na Kijamii kwa kuzingatia kuimarisha Uwazi, Uwajibikaji na Ukuzaji  Uchumi.

Naye bwana Donald Ria ambaye ni Mtaalamu Mshauri wa masuala ya mazingira ya biashara na uwekezaji kutoka Mradi wa kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya serikali ya Denmark na Tanzania alisema kuwa mradi wake ulikubali kufadhili kuandaliwa kwa mwongozo huo ili kuboresha ukusanyaji wa mapato katika halmashauri.

 

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *