Video

TAMISEMI Yaendelea Kuwabaini Watoto Wenye Mahitaji Maalum

Na. Fred Kibano

Mratibu wa Sehemu ya Elimu Maalum Ofisi ya Rais TAMISEMI, Julius Migea amesema Serikali imeanzisha Mpango wa stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) kwa watoto wenye mahitaji maalum ili kuwabaini na kuwawezesha kumudu stadi hizo muhimu kwa maendeleo yao na Taifa.

Migea aliyasema mjini Dodoma wakati wa kuanza rasmi kwa zoezi hilo lenye lengo la kuwabaini watoto wenye mahitaji maalum kama uoni hafifu, viungo vya mwili, kutosikia, kushindwa kuongea na matatizo mengine.

“Mpango huu wa kukuza stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) ulianzishwa kwa lengo la kukabiliana na kiwango duni cha kumudu stadi hizo za msingi kilichobainika miongoni mwa wanafunzi wa shule za msingi nchini, na watoto waliolengwa ni wenye umri kati ya miaka mine hadi sita”

Migea alisema kuwa uendeshaji wa uchunguzi wa nchi nzima kwa watoto wenye umri wa miaka 4 hadi 6 ni kwa ajili ya kuwabaini watoto wenye mahitaji maalum ili waweze kupatiwa afua stahiki ikiwa ni pamoja na kuwaandikisha shule stahiki. Kwa hivi sasa, tayari timu za maafisa waliopewa mafunzo maalum zimekwisha kwenda katika mikoa na halmashauri zote nchini na wameanza kuwabaini watoto hao wenye mahitaji maalum wanaoishi katika kata, vijiji, vitongoji na mitaa.

Mmoja wa wataalam wa kubaini watoto wenye mahitaji maalum, Suleimani Kingo akimpima mtoto mwenye tatizo la kuongea wakati wa uendeshaji wa zoezi hilo katika Halmashauri ya wilaya Kondoa kata ya Pahi
Mtaalam wa kubainisha watoto wenye mahitaji maalum, Julieth Philipo akipata maelezo ya mtoto mwenye tatizo la uoni hafifu wakati wa uendeshaji wa zoezi hilo katika Halmashauri ya wilaya Kondoa kata ya Pahi.

Naye Mratibu wa kazi ya kubaini watoto wenye mahitaji maalum Stephen Mwendi amesema zoezi la kubaini watoto wenye mahitaji maalum mkoani Dodoma linaendelea vizuri katika wilaya ya Kondoa Mji na Halmashauri ya Kondoa, baada ya kumaliza Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma na baada ya hapo watakwenda katika halmashauri nyingine za mkoa wa Dodoma.

Serikali imekuwa ikitekeleza Mipango mbalimbali katika sekta ya elimu, ambapo kwa hivi sasa kupitia Mpango wa Kukuza stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (Literacy and Numeracy Education Support – LANES) inatekeleza mikakati ya kuhakikisha wanafunzi wote walioandikishwa shule za Msingi wanapata stadi za KKK ambazo ni msingi muhimu wa maendeleo ya kitaaluma katika ngazi zingine za Elimu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *