Habari za Wizara

TAMISEMI yaridhishwa na miradi Jiji la Arusha

Mhandisi wa ujenzi Halmashauri ya Jiji la Arusha, Bw.August Mbuya (katikati) akiongoza timu ya wataalamu kutoka Ofisi ya Rais ,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) inayohusika na ufatialiaji na tathmini kukagua mradi wa barabara ya Sombetini Ngusero ambayo imejengwa kupitia Mradi wa Uboreshaji Miji (TSCP).

Na. Angela Msimbira OR-TAMISEMI Arusha

Timu ya wataalamu kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa( OR TAMISEMI) imeridhishwa na ujenzi wa miradi ya uboreshaji miji nchini katika Halmashauri ya Jiji la Arusha unaotekelezwa na fedha za mkopo wa benki ya dunia.

Mratibu wa Ujengaji uwezo kitaasisi wa miradi hiyo Bi. Debora Mkemwa amesema lengo la ziara hiyo ni kuratibu na kufuatilia maendeleo ya Miradi ya Uboreshaji Miji inayotekelezwa na Halmashauri ya Jiji la Arusha.

Amesema kuwa miradi itakayotembelewa na timu hiyo ni ujenzi wa barabara ya Sombetini –Ngusero yenye urefu za zaidi ya kilometa 2 pamoja na ujenzi wa uwanja wa michezo kwa watoto eneo la Shule ya Msingi Ngarenaro utakaotoa fursa ya kuibua vipaji katika umri mdogo.

Bi. Mkemwa amewaagiza viongozi wa Halmashauri hiyo  kuhakikisha ujenzi wa uwanja huo ambao utakua na sehemu mbalimbali za michezo kuzingatia kanuni za usalama ili kuwalinda wanafunzi wa Shule ya Msingi na Sekondari Ngarenaro na wananchi waelimishwe manufaa ya mradi huo utakapokamilika.

Bi.Mkemwa ameongeza kuwa anatarajia miradi hiyo itatoa huduma kwa wananchi na itakua chanzo kizuri cha mapato kwenye halmashauri ambako miradi hiyo inatekelezwa.

Naye Mchumi Mwandamizi kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Bw. Adam Mbeyela amesema fedha zilizotolewa kwa awamu tatu zimesaidia miradi mbalimbali nchini kujengwa kwa upande wa jiji la Arusha ujenzi wa uwanja wa michezo ya watoto,dampo kuu eneo la Muriet na ujenzi wa barabara .

Amesema katika awamu ya pili ya utoaji fedha mradi huo wa ujenzi umefikia asilimia 63 kati ya 70 iliyotarajiwa na itakua na matokeo chanya baada ya kukamilika.

Wakati huohuo Mhandisi wa ujenzi halmashauri ya Jiji la Arusha, Bw.August Mbuya amesema shughuli za ujenzi zinaendelea vizuri na anatarajia zitakamilika katika kipindi kilichokubaliwa.

Mhandisi wa ujenzi Halmashauri ya Jiji la Arusha Bw.August Mbuya akiwapa maelezo wataalamu kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) inayohusika na ufuatialiaji na tathmini kuhusu Miradi ya barabara ya Sombetini Ngusero ambayo imejengwa kupitia mradi wa uboreshaji miji (TSCP).
Mratibu wa Ujengaji uwezo kitaasisi wa miradi inayofadhiliwa na mikopo kutoka Benki ya Dunia, Bi. Debora Mkemwa (kushoto) akizungumza wakati timu ya wataalamu kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) inayohusika na ufuatialiaji na tathmini ilipokagua mradi wa ujenzi wa uwanja wa michezo ya watoto Shule ya Msingi Ngarenaro Jijini Arusha.

 

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *