Habari za Kiuchumi/Kilimo

Tumieni Kituo cha Biashara Kukuza Uchumi – Nzunda

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI Tixon Nzunda akiangalia ukaushaji wa dagaa-kigoma katika mwalo wa Kibirizi Manispaa ya Kigoma huku Afisa Mifugo na Uvuvi wa Manispaa hiyo Bw.Aziz Daud akifafanua jambo, kulia mwenye tai ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma Rashid Mchanga

Na Fred Kibano

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa – ELIMU (OR TAMISEMI) Tixon Nzunda, ameagiza kuanza kutumika kwa kituo cha huduma za biashara (one stop business centre) ifikapo mwishoni mwa mwezi huu bila kusubiri uzinduzi rasmi.

Nzunda ametoa kauli hiyo leo wakati akikagua miradi ya maendeleo katika halmashauri za Manispaa na Wilaya Kigoma na kuwataka Watendaji kuanza kutumia kituo hicho ili kuleta huduma kwa wananchi na kuongeza mapato ya Halmashauri hizo kama ilivyolengwa. 

“natumaini mwaka huu, mwisho wa mwezi huu tarehe 01.12.2018, kituo hiki kitaanza kufanya kazi zake kama tulivyokubaliana, Katibu Tawala hili ulisimamie, haiwezekani fedha nyingi zimetumika kujenga jingo hili na halitumiki kama ilivyokusudiwa”

Amesema idara za Ardhi, Biashara, Afya, Mamlaka ya Mapato Tanzania, Idara ya Uhamiaji na nyinginezo zihamie mara moja na kutumia jengo hilo ili kutoa huduma bora kwa wananchi.

Katika hatua nyingine Nzunda amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri za Kigoma Manispaa na Kigoma kuchukua hatua za kinidhamu kwa watumishi waliopoteza mashine za kukusanyia mapato ‘point of sales machine’ ambapo amewaagiza kuwa watumishi waliopoteza wawajibike kwa kulipa na kwa sasa zinunuliwe wakati utaratibu wa kuwakata unafanyika.

Kwa upande wake Mwailwa Pangani Mkurugenzi wa Kigoma Manispaa amesema jumla ya shilingi 699,000,000 zilitolewa na Mradi wa Kuboresha Mazingira ya Biashara (Locasal Investment Climate) na kufanikiwa kujenga na kuboresha mradi wa mwalo ili kupunguza upotevu wa mazao ya uvuvi na kuongeza kipato kwa wavuvi na halmashauri ya Manispaa Kigoma.

Naye Upendo Mangali ambaye ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Kigoma amesema Mradi wa uwekezaji wa shughuli za kiuchumi kwa jamii (Local Investment Climate) LIC unaowezeshwa na Wadau umesaidia kuwepo kwa mabaraza ya biashara ya wilaya ili kukuza uchumi, kuwa na utaratibu wa ukusanyaji wa mapato kwa kutumia mfumo wa mapato ujulikanao kama LGRCIS ambao Programu ya LIC wamegharamia katika kuweka pamaoja na ufadhili wa vifaa wilayani Kigoma na pia ujenzi wa miundo mbinu katika soko la Kalinzi (Kalinzi )

Mangali amesema makusanyo ya mapato yameongezeka ambapo katika kipindi cha mwaka wa fedha 2017/2018 mapato yalikuwa shilingi 10,200,840 bila kutumia mfumo na kwa sasa ni shilingi 30,000,000 hali ambayo imeongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato

Katika ziara yake Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI ametembelea soko la Mwanga (Mwanga Night Market), soko la Kampuni ya Uendeshaji Mwaro wa Kibirizi linalosimamiwa na Kibirizi Landsite Company LTD na kuongea na watumishi na watendaji wa Mamlaka zote mbili.

Mradi wa Kuboresha Mazingira ya Biashara (Locasal Investment Climate) unafadhiliwa na Wadau wa Maendeleo na unalengo la kuboresha huduma na mazingira ya biashara kwa wananchi na halmashauri ili kuinua kipato cha mwananchi wa kawaida.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *