Habari za mikoani

Ubalozi wa Japan Kujenga Sekondari Keikei Kondoa

 

Na. Sekella Mwasubila- H/Mji Kondoa

Ubalozi wa Japan umeahidi kujenga Shule ya Sekondari ya kata ya Keikei ili kupunguza mrundikano wa wanafunzi katika Shule ya Sekondari ya kata ya Busi inayohudumia wanafunzi wa kata mbili.

Ahadi hiyo ilitolewa na mwakilishi wa ubalozi wa Japan Bwana Takao Kurukawa katika kata ya Keikei alipofika katika eneo lililotengwa  kwaajili ya ujenzi wa sekondari hiyo hivi karibuni.

“Nimekuja kuangalia eneo ambalo litajengwa Shule ya  Sekondari na ubalozi wa Japan baada ya kupokea maombi ya kuomba kujengewa shule kutoka Halmashauri ya Wilaya  ya Kondoa “Alisema Bwana Takao

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kondoa Mhe. Sezeria Makota aliwashukuru ubalozi wa Japan kwa msaada wao na kuwataka wananchi wa Keikei kujitoa kwa hali na mali ila kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati na kuwahudumia wananchi.

“Shukrani za dhati ziende kwa Mbunge Mhe.Ashatu Kijaji kutokana na agenda yake ya kuhamasisha elimu na sasa anatekeleza kwa vitendo baada ya kuona watoto wengi wanafaulu na kwenda shule ya Sekondari Busi hali iliyopelekea kuwa na upungufu wa madarasa hivyo mheshimiwa mbunge akaamua kwenda kuomba msaada ubalozi wa Japan na leo wamekuja.” Alisema Mhe.Makota

Hata hivyo Mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Kondoa Mustapha Semwaiko alisema kuwa katika Kata 21 za Halmashauri ya Wilaya  ya Kondoa ni Kata ya Keikei pekee ambayo haikuwa na Sekondari ya Kata na kulikuwa na ufaulu mkubwa wa wanafunzi ambao ulisababisha msongamano katika Sekondari ya Busi na kupelekea kuwe na upungufu wa madarasa.

“Kutokana na kuwa na tatizo la madarasa Shule ya Sekondari ya Busi tulishirikiana na  Mheshimiwa Mbunge tukapiga hodi katika ubalozi wa Japan ambao walikubali na watatujengea madarasa 8, matundu ya vyoo 10 na ofisi 2 za walimu na sisi tumetenga eneo la ekeri18 kwaajili ya ujenzi wa shule hiyo.”Alisisitiza Mustapha

Mmoja wa wananchi wa Kata hiyo Bwana Juma Ramadhani aliwashukuru viongozi wote walioshiriki katika kufanikisha jambo hilo kwa kuwa watoto wao walikua wakitembea umbali mrefu kufuata Sekondari katika kata jirani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *