Habari za Kiuchumi/Kilimo

USAID – Feed the Future Wakabidhi gari Ofisi ya Rais TAMISEMI

 

Mkurugenzi Msaidizi wa Shirika la Misaada USAID anayehusika na kukuza uchumi Michelle Corzine, akimkabidhi  Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango Ofisi ya Rais TAMISEMI John Cheyo kwa niaba ya Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI, funguo ya gari aina ya Toyota Land Cruiser  leo katika jengo la Mkapa Jijini Dodoma.
Mkurugenzi Msaidizi wa Mradi wa Maendeleo ya vijana ‘Feed the Future’ Inua Vijana Tanzania, Bi Ngasuma Kanyeka akisaini Mkataba wa makubaliano ya ushirikiano na  Ofisi ya Rais TAMISEMI leo Jijini Dodoma. Kushoto kwake ni Dkt. Andrew Komba Mkurugenzi wa Sera na Mipango Ofisi ya Rais TAMISEMI.

Na. Magdalena Dyauli na Ainess Makassi

Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali Mitaa (TAMISEMI), imekabidhiwa gari aina ya Toyota Land Cruiser na Mradi wa kuinua vijana Tanzania ‘Feed the Future’ uliochini ya Shirika la Misaada la Marekani USAID.

 Makabidhiano hayo yamefanyika leo Jijini Dodoma katika Ofisi ya Rais – TAMESEMI ambapo Mkurugenzi wa Sera na Mipango John Cheyo alipokea gari hilo kwa niaba ya ofisi hiyo.

Mradi huo wa maendeleo ya vijana unaendeshwa katika mikoa iliyopo Zanzibar na mikoa ya Mbeya na Iringa na una lengo la kuendeleza vijana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 35 katika Nyanja mbalimbali zikiwemo Uchumi, Uongozi, Stadi za maisha pamoja na Afya. 

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Msaidizi wa Mradi huo Bi. Ngasuma Kanyeka, alisaini Mkataba wa makubaliano ya ushirikiano kati ya USAID Feed the Future na Ofisi ya Rais TAMISEMI ambayo pia alisaini Katibu Mkuu Mhandisi Mussa Iyombe.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu wa Kisekta Ofisi ya Rais TAMISEMI, Dkt Andrew Komba alishukuru Mradi huo kwa msaada wa gari kwani utapunguza tatizo la usafiri na amewataka Wadau hao kuendelea kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI katika sekta mbalimbali zikiwemo Elimu, Afya, Uchumi pamoja na Uzalishaji mali.

“naomba tuendeleze ushirikiano, muendelee kuona mnalo jukumu la msingi kubadilisha maisha ya watanzania” alisema Dkt. Komba

Aliongezea kuwa USAID inashirikiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI katika maandalizi ya Sera ya Ung’atuaji wa Madaraka ambayo ipo katika mchakato wa kuandaliwa. Alisema shirika hilo linasaidia kutoa utaalamu pamoja na fedha zakuwezesha mchakato mzima wakupata sera hiyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa shirika la Maendeleo la Marekani USAID Michelle Corzine anayehusika na kukuza uchumi Tanzania, alisema shirika hilo linashirikiana na Serikali ya Tanzania kusaidia vijana na hadi sasa vijana 1,600 wamefaidika na mradi huo.

Ofisi ya Rais TAMISEMI inashirikiana na Wadau mbalimbali wa Maendeleo kwa lengo la kuwaletea Wananchi maendeleo kama inavyoelekezwa na Serikali ya Awamu ya Tano na Chama Tawala.

                                                                

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *