Elimu

Ushirikiano wa Serikali na Wadau Utainua ELIMU nchini – Nzunda

 

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) – anayeshughulikia Elimu Tixon Nzunda akifungua kikao kazi leo mjini Mwanza cha kuandaa vipindi vya redio kupitia Mpango wa Kuinua Ubora wa Elimu Tanzania (MKUE-Tanzania)

Na. Fred Kibano

SERIKALI imetoa wito kwa Wadau wa elimu kushirikiana na Serikali katika kujenga mazingira mazuri ya utoaji wa elimu nchini ikiwa ni pamoja na ujenzi wa madarasa, vyoo na nyumba za walimu.

Kauli hiyo imetolewa leo mjini Mwanza na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) – anayeshughulikia Elimu Tixon Nzunda wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha kuandaa vipindi vya redio kupitia Mpango wa Kuinua Ubora wa Elimu Tanzania (MKUE-Tanzania).

Alisema hali ilivyo sasa ili kukamilisha miundombinu na kuweka mazingira mazuri ya utoji wa elimu na ujenzi wa nyumba za kuishi walimu kwani bado zinahitajika shilingi trilioni 14 kutekeleza zoezi hilo katika Shule za Sekondari na Msingi nchini kote na kwamba mchnago wa Wadau bado unahitajika.

Nzunda amesema Serikali pekee haiwezi kukamilisha zoezi hilo bila kushirikiana na wadau wengine ili kujenga madarasa ya kutosha na kupunguza msongamano wa wanafunzi, kuondoa uhaba wa nyumba za walimu, vyoo na miundombinu mingine.

Alisema Serikali katika kukabiliana na tatizo la msongamano wa wanafunzi katika shule mbalimbali za Msingi na Sekondari tayari katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita imetoa zaidi ya shilingi bilioni 65 kwa ajili ya ujenzi wa maboma ya madarasa yapatayo 5,289 nchini kote.

Nzunda amesema kuwa fedha hizo zimesaidia kukamilisha maboma 2,392 kwa ajili ya Sekondari na 2,897 ni kwa ajili ya Msingi nchini kote.

Baadhi ya waandishi wa habari, Maafisa Elimu Mikoa na Maafisa Habari wakiwa katika mafunzo ya siku tatu ya kuandaa vipindi vya redio mjini Mwanza leo.

Katika hatua nyingine Nzunda amesema kuwa badala ya Asasi zisizo za Kiserikali (NGOs) kutumia fedha katika utetezi (Advocacy) unaonyesha na kutangaza changamoto na mapungufu katika Shule nchini kama vile msongamano na upungufu wa matundu ya vyoo mashuleni ni vema wakatumia fedha hizo kushirikiana na Serikali katika kuboresha mazingira ya Shule nchini.

Aidha, Nzunda amewapiga marufuku walimu wanaofundisha madarasa ya kuanzia elimu ya awali hadi darasa la tatu kuingia na viboko madarasa kwani kitendo hicho kinasababisha wanafunzi wa madarasa hayo kuogopa na kutokuwa wasikivu wakati wa wanapofundishwa.
Kuhusu Mpango wa Kuinua Ubora wa Elimu Tanzania (MKUE-Tanzania) alisema kuwa umechangia katika kuboresha elimu katika mikoa 9 kiwango cha ufaulu kwa shule za Msingi umeongezeka kutoka chini asilimia 40 hadi kuwa juu ya 77 na maeneo mengine kufikia asilimia 100.

Mafunzo hayo ya siku tatu kupitia Mpango wa Kuinua Ubora wa Elimu Tanzania (MKUE-Tanzania) yanayowashirikisha waandishi wa habari, Maafisa Elimu Mikoa na Maafisa Habari kutoka Mikoa 9 yameandaliwa na TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Maendeleo ya Kimataifa ya Uingereza(DFID).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *