Habari Kitaifa

Ushirikiano wa Viongozi na Watumishi Utaboresha Huduma kwa Wananchi

Na Majid Abdulkarim na Fred Kibano

 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo akitoa hotuba wakati wa hafla ya kuwaaga Viongozi na kuwakaribisha Viongozi wapya wizarani OR TAMISEMI Jijini Dodoma
Baadhi ya watumishi wa OR TAMISEMI wakisikiliza hotuba ya Waziri wa Nchi OR TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo wakati wa  hafla ya kuwaaga Viongozi na kuwakaribisha Viongozi wapya iliyofanyika wizarani hapo OR TAMISEMI Jijini Dodoma

Watumishi wa Umma wametakiwa kutumia sheria, taratibu, kanuni na busara katika kutekeleza majukumu ili kuleta ubora katika huduma wanazo zitoa kwa watanzania.

Hayo yamebainishwa leo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) Selemani Jafo katika hafla fupi ya kuwakaribisha Viongozi wapya na kuwaaga Viongozi waliokuwa katika ofisi hii.

Mhe. Jafo amesema ili kupata matokeo bora katika utendaji kazi wa mtumishi yeyeto lazima kujenga daraja la mahusiano mazuri na upendo baina yetu ili kuweza kutoa huduma stahiki kwa watanzania tunao wahudumia.

“Sisi Viongozi jukumu letu ni kuwahudumia watanzania na kuhakikisha wanapata huduma bora kutoka kwetu kwani wao ndio walio tupa dhamana hii ya kuwatumikia, bila wao sisi tusingekuwa na watu wa kuwahudumia” Amesema Jafo.

Jafo amesema kuwa yeye na timu nzima ya Ofisi ya Rais -TAMISEMI wanawakaribisha Katibu Mkuu OR – TAMISEMI Mhandisi Joseph Nyamhanga na Naibu Katibu Mkuu (Afya) OR-TAMISEMI Dkt. Dorothy Gwajima na kuwaahidi kutoa ushirikiano wa hali ya juu ili kuhakikisha wanapata matokeo zaidi katika utendaji kazi wa kuwahudumia wananchi.

Jafo ameongeza kuwa kuna haja ya Katibu Mkuu OR-TAMISEMI Mhandisi Joseph Nyamhanga kukaa na wataalamu wake kuona ni namna gani wataboresha miundo mbinu ya barabara katika Halmashauri na Wilaya za nchi hii.

Kwa upande mwingine Jafo amesema kuwa anawapongeza sana Mhandisi Mussa Iyombe na Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt.Zainabu Chaula kwa ushirikiano mzuri na utendaji bora waliyouonyesha kipindi walichohudumu katika Ofisi ya Rais – TAMISEMI na kuwatakia kila la kheri huko waendako.

Naibu Waziri anayeshughulikia Elimu OR – TAMISEMI George Mwita Waitara amewataka watumishi kuwa mabalozi wazuri wa Serikali katika kutekeleza miradi mbali mbali inayotekelezwa na serikali hii.

“Kila mtumishi ni wajibu wake kuwa muadilifu katika kutekeleza miradi ya Umma na kila mtu atambue wajibu wake katika nafasi yake ili kuleta mapinduzi katika kukuza maendeleo ya nchi yetu” Amesema Waitara.

Kwa upande wake Katibu Mkuu OR – TAMISEMI Mhandisi Joseph Nyamhanga ametoa wito kwa watumishi wa OR-TAMISEMI kumpa ushirikiano wakutosha katika kuboresha huduma za utekelezaji wa miradi ya Umma, kusimamia ukusanyaji wa mapato na kuhakikisha yanatumika vizuri katika kuwanufahisha watanzania kwani ni kodi zao.

Akitoa neno la kuwaaga na kuwashukuru watumishi na Viongozi wa OR TAMISEMI, Mhandisi Mussa Iyombe ametoa nasaha kwa watumishi wa Umma kwa kuwataka kutenda haki na kuwa wawazi katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku kwani ndio silaha bora ya mtumishi Umma.

Naye Dkt.Chaula ametoa wito kwa watumishi wote kuwa na utayari wa kufanya kazi na mtu yeyote na sehemu yoyote kwani watumishi jukumu kubwa kwao ni utendaji na katika swala la uongozi ni mchezo wa kupokezana vijiti.

Awali akiwasalimia watumishi wa OR TAMISEMI Dkt. Dorothy Gwajima amesisitiza kuimarisha uratibu mzuri, uwazi, utekelezaji wa majukumu ili kujenga Serikali ya watu na kwa ajili ya maendeleo ya watanzania kwa ujumla.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *