Habari za Wizara

Vituo vya afya vyatakiwa kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia afya Dkt. Zainabu Chaula akisisitiza jambo kwa uongozi wa Mkoa wakati  alipotembelea kituo cha afya cha Tinde kilichopo katika Mkoa wa Shinyanga wakati akiwa njiani kuelekea Geita kwenye ziara ya kikazi ya kukagua ukarabati na ujenzi wa vituo vya afya nchini.

 

Na. Angela Msimbira OR-TAMISEMI, SHINYANGA

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia afya Dkt. Zainabu Chaula  amewaagiza  Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya Nchini kuhakikisha wanasimamia ukusanyaji wa mapato kwenye vituo vya afya  ili kuongeza mapato na kujiendesha vyenyewe.

Dkt. Chaula ameyasema hayo alipotembelea kituo cha afya cha Tinde  kilichopo Mkoani Shinyanga wakati  akiwa njiani  kuelekea  Mkoa wa Geita  kwenye ziara yake ya kikazi ya kukagua maendeleo ya ukarabati na ujenzi wa vituo vya  afya nchini.

Amesema kuwa Serikali imejenga miundombinu bora ya vituo vya afya nchini kwa gharama kubwa  hivyo ni vyema Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha wanakusanya mapato ili vituo hivyo viweze kujiendesha  vyenyewe.

“Serikali imewekeza fedha nyingi katika ujenzi wa miundombinu ya afya nchini lakini inasikitisha kuona bado kasi ya ukusanyaji wa mapato ndogo, nawaagiza Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha mnaongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato kwenye Vituo vya afya vyote nchini“ Anasisitiza Dkt. Chaula

Dkt. Chaula amewataka Wanganga hao kubuni mikakati  itakayosaidia kuongeza mapato na kuhakikisha wanafunga mfumo wa kielektroniki wa ukusanyaji wa mapato katika vituo vyote vya afya nchini na kuhakikisha wanawasiamamia watumishi kuutumia mfumo huo kwa uaminifu mkubwa.

Akiongelea kuhusu maendeleo ya ujenzi wa vituo vya afya nchini ameupongeza uongozi wa Serikali  ya Mkoa wa shinyanga kwa kusimamia  ujenzi huo kwa weledi mkubwa na kusababisha kituo cha afya cha Tinde kukamilika kwa wakati.

Amewaagiza viongozi hao kuhakikisha wanasimamia upandaji wa Miti ya matunda katika maeneo ya kituo cha afya cha Tinde ili kupendezesha mandhari ya eneo hilo na kuwa kivutio kwa wagonjwa wanaokuja kupata huduma katika kituo hicho.

“Vituo vya afya vyote nchini vinatakiwa kuhakikisha vinaweka mazingira safi na kutengeneza mandhari ya maeneo kwa kupanda miti  ya matunda ili wagonjwa wanapokuja kutibiwa wavutike na mazingira yaliyopo” Anasema Dkt. Chaula

Aidha amewataka  wasimamizi wa maeneo kuhakikisha  wanaanzisha kampeni ya Usafi wa mazingira na kuachana na dhana ya kufanya usafi  wa maeneo baada  ya kukamilika  kwa shughuli za ujenzi.

Jengo la wodi ya wazazi lilijengwa katika kituo cha afya cha Tinde kilichopo Mkoani Shinyanga.

 

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia afya Dkt. Zainabu Chaula akisikiliza maelezo  wakati alipotembelea Kituo cha afya cha Tinde kilichopo katika Mkoa wa Shinyanga  akiwa njiani kuelekea Geita kwenye ziara ya kikazi ya kukagua ukarabati na ujenzi wa vituo vya afya nchini

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *