Habari za Wizara

Waganga Vituo vya afya, Wakuu wa shule jifunzeni elimu ya uhasibu

Na Mathew Kwembe, Kagera
Waganga Wafawidhi wa Vituo vya Afya, Zahanati na Walimu Wakuu wa Shule za Msingi na Sekondari wanaopelekewa fedha na serikali moja kwa moja kwenye vituo vyao wametakiwa kujifunza elimu ya uhasibu ili waweze kutekeleza majukumu yao uafisa masuuli ya usimamizi wa fedha za serikali.

Ushauri huo umetolewa jana na Meneja wa Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma wa Mkoa wa Kigoma bwana Simon Mabagala wakati wa mahojiano maalum kuelezea alichojifunza kuhusu watendaji hao wa ngazi za chini wa Mamlaka za Serikali za Mitaa wanavyotekeleza majukumu yao kupokea fedha na kupitisha maamuzi ya matumizi ya fedha hizo kwa kupitia mfumo huo wa kielekitroniki.

Alisema kuwa baadhi ya walimu wakuu na waganga wafawidhi wamekuwa wakisita kutekeleza jukumu hilo uhasibu kwa kuwa taaluma zao ni tofauti lakini kutokana na uamuzi huo wa serikali wa kupeleka fedha moja kwa moja katika vituo vyao watalazimika kujifunza elimu ya uhasibu ili waendane na majukumu yao ya uafisa masuuli katika vituo vyao.
Bwana Mabagala aliongeza kuwa watendaji hao hawawezi kukwepa kujifunza elimu ya uhasibu kwani kwa jukumu lao la uafisa masuuli wasipoweza kuwa na elimu ya uhasibu kidogo wanaweza kushindwa kutekeleza majukumu yao.

“Kwa kuwa msimamizi wa kituo moja kwa moja wewe ni afisa masuuli, unalazimika kufahamu mambo ya msingi ya uhasibu kwani kushindwa kufahamu majukumu maana yake hela wasikuletee, kwani serikali haiwezi kukuletea hela, wakati wewe ndiyo msimamizi wa kituo, ni lazima uweze kuzisimamia na kuzitolea taarifa,” alisema.
Kwa upande wake Mhasibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kahama bwana Edwin Lupili alieleza kuwa katika halmashauri yake vituo vyote vya afya vimeletewa wahasibu, hivyo suala la kupeleka fedha moja kwa moja katika vituo hivyo linafanyika bila tatizo kwa kuwatumia wahasibu.
Aliongeza kuwa katika shule za msingi na sekondari kumekuwa na changamoto za kupata wahasibu watakaotosheleza vituo hivyo hasa kwa kuzingatia kuwa idadi ya shule za msingi nchini ni zaidi ya 16,000 na shule za sekondari ni zaidi ya shule 3600.
Sababu nyingine ya kutolazimika kuweka mhasibu kwa kila shule ni kutokana na kiwango cha fedha kinachopelekwa katika shule hizo kutokuwa kikubwa kiasi cha kuhitaji kuajiri mhasibu kwa kila shule.
Bwana Lupili aliongeza kuwa pamoja na serikali kutokuajiri wahasibu wanaoweza kukidhi mahitaji ya kila shule nchini, bado walimu wakuu na waganga wa vituo vya afya wana fursa ya kupata msaada wa kitaalamu kupitia miongozo ya serikali ambayo imeainisha mchanganuo wa matumizi wa fedha zinazopelekwa kwenye vituo.

Pia alisema kuwa zipo kamati za shule na afya ambazo zimekuwa zikipigwa msasa kuhusu mambo ya uhasibu na hivyo kusaidia jukumu la usimamizi na udhibiti wa matumizi ya fedha za serikali zisitumike kinyume na miongozo kwenye vituo hivyo.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *