Habari za mikoani

  Waitara Aweka Rekodi Njombe, Apongeza Ujenzi wa Miradi Afya,Elimu

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kambarage Halmashauri ya Mji Njombe akiwa ameambata na Naibu Waziri TAMISEMI Mwita Waitara katika ukaguzi wa shughuli za ujenzi wa vyumba 4 vya madarasa kwenye shule hiyo

Hyasinta Kissima-Afisa Habari H/Mji Njombe

 Naibu Waziri Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Mwita Waitara amezuru katika Halmashauri ya Mji Njombe kukagua shughuli mbalimbali za Maendeleo huku akitoa pongezi kwa uongozi wa Halmashauri hiyo baada yakuridhishwa na hali ya miradi  na hatua zilizofikiwa kwa sasa.

Akiwa katika ziara hiyo, Waitara ametembelea na kukagua ujenzi wa Kituo cha Afya Makowo, Ujenzi wa Madarasa katika Shule ya Msingi Makowo Kata ya Makowo pamoja na shule ya Msingi Kambarage zilizopo Halmashauri ya Mji Njombe.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa mbele ya kiongozi huyo, serikali ilitoa zaidi ya shilingi Milioni 72.5 za kitanzania ili kufanikisha ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule hizo, kufuatia hatua za ujenzi zinazoendelea na mafanikio waliyofikia ilimlazimu kiongozi huyo kuipongeza Halmashauri na Wananchi kwa ujumla kwa kushiriki wao wa pamoja katika utekelezaji wa miradi hiyo.

“Serikali imetoa fedha kwa ajili ya kuanzisha, kuboresha na kusimamia miradi ya maendeleo ili kuhakikisha kuwa kero za wananchi zinatatuliwa. Zipo Halmashauri ambazo zimekuwa zikitekeleza miradi ya maendeleo hewa. Fedha zinapelekwa katika maeneo husika lakini miradi haipo. Wakati mwingine mradi haulingani na thamani ya fedha iliyotumika” alisema Waitara.

Ameongeza kuwa, Serikali ilishatoa maelekezo juu ya fedha zinazopelekwa kwa wananchi zitumike kwa malengo ya miradi husika tu kwakuwa kinachofanyika nikwa niaba ya Rais hivyo matamanio na Falsafa ya Mheshimiwa Rais vema vikapewa kipaumbele.

Awali akizungumza na Watumishi kutoka katika Halmashauri ya Mji Makambako, Halmashauri ya Mji Njombe na Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, Waitara amewataka watumishi kuhakikisha wanafanya kazi kwa weledi na kuzingatia kanuni za Utumishi wa umma huku akiwataka Watumishi kuwatembelea na kutoa huduma kwa wananchi katika maeneo yao.

Kwa upande wao wananchi wa Kata hiyo wameipongeza Serikali kwa hatua ambazo imekuwa ikizichukuwa za  kuimarisha shughuli za maendeleo na kuhakikisha kuwa viongozi wanawafikia Wananchi hata katika maeneo ya vijijini  huku wakimpongeza Naibu Waziri Waitara kwakuvunja rekodi ya kuwa Naibu Waziri wa Kwanza kufika katika Kijiji hicho.

“Katika maisha yetu yote hatujawahi kupokea ugeni kama huu. Wewe ni Naibu Waziri wa kwanza kufika katika Kata hii umevunja   rekodi, kwa kweli tumefarijika sana” Alisema Diwani wa Makowo Mhe. Mgaya.

Naibu Waziri Waitara yupo katika ziara ya kikazi katika Mkoa huo, ikiwa ni sehemu ya Ziara yakukagua shughuli mbalimbali za Maendeleo ikiwa ni mkakati wakutambua juhudi zinazo chukuliwa na Serikali kwenye kuwahudumia wananchi.

Mganga Mkuu Halmashauri ya Mji Njombe Dkt. Thomas Ndalio akisoma taarifa ya shughuli za ujenzi zinazoendelea katika  Kituo Kipya cha Afya kinachojengwa katika Kata ya Makowo ujenzi unaofanywa kupitia nguvu za Wananchi, Halmashauri na Mfuko wa Jimbo
Sehemu ya Wananchi kutoka Kata ya Makowo waliokusanyika kumsikiliza Naibu Waziri TAMISEMI Mwita Waitara mara baada ya kuwasili na amewaahidi kuwasaidia upatiokanaji wa vifaa tiba vya muhimu mara baada ya kukamilika kwa kituo cha afya Makowo
Diwani wa Kata ya Makowo Honoratus Mgaya akizungumza mbele ya Naibu Waziri mara baada ya kupokea ugeni huo ulijiri kwa ziara ya siku moja na kujionea shughuli za Maendeleo katika Kata hiyo.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *