Habari za Wizara

Wajumbe wa ALAT Wapata somo la Mifumo

Erick Kitali Mkurugenzi wa TEHAMA, OR TAMISEMI, akiwasilisha mada kuhusu mifumo ya TEHAMA wanayo ihudumia na umuhimu wake katika juhudi za kusukuma maendeleo ya nchi.

Na. Atley Kuni- OR TAMISEMI

Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania Bara (ALAT), wamepata somo juu ya mifumo inayo simamiwa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR TAMISEMI) na jinsi mifumo hiyo ilivyo saidia katika masuala mtambuka ya kimaendeleo katika jamii.

Somo hilo limetolewa na Mkurugenzi wa TEHAMA OR TAMISEMI, Ndugu Erick Kitali wakati wa Mkutano Mkuu wa 34 wa Jumuiya hiyo unaoendelea mkoani Dodoma na kuwakutanisha wajumbe kutoka Halmashauri 185 za Tanzania Bara.

Akitoa mada hiyo Mkurugenzi huyo wa TEHAMA, alisema toka kuanza kwa mifumo mambo mengi yameimarika ikiwepo suala la mapato ya halmshauri ambapo kupitia mfumo wa ukusanyaji wa mapato ya ndani ya Halmashauri (Local Government Revenue Collection Information System- LGRCIS), imewezesha halmashauri hizo kujiongezea mapato ya ndani ikilinganishwa na hapo awali.

“Waheshimiwa wajumbe, kupitia mifumo yetu hali ya makusanyo imeongezeka sana ikilinganishwa na kipindi cha nyuma ambacho tulikuwa tunakusanya kwa risiti za kawaida” alisema Kitali, na kutolea  mfano katika maeneo yetu ya kutolea huduma za afya hususan ni katika Hospitali za Wilaya ambapo makusanyo yalikuwa kati ya Mil. 3 hadi 6 kwa mwezi, lakini pindi matumizi ya mifumo yalipoanza, makusanyo yamepanda na kufikia Mil. 24 hadi 40 kwa mwezi.

Kwa upande wao wajumbe hao wakichangia na kutoa ushauri walipongeza kazi nzuri inayofanywa na wizara ya OR-TAMISEMI, huku wakitaka maboresho ya mtandao katika mifumo hiyo iweze kuongeza ufanisi hasa katika maeneo ya pembezoni mwa nchi, ambapo mkonga wa taifa bado haujafika.

Akichangia mada Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Wakili Kiomoni Kiburwa Kibamba, alisema katika kuimarisha suala zima la Makusanyo Serikali iende mbele na kuwa na mawazo mbadala juu ya (Point of Sell- POS).

“Mhe. Mwenyekiti nadhani umefika wakati wa kuwa na mashine hizi za POS ambazo zitakuwa zinajazwa Flot ili kusaidia kuepusha hatari mbali mbali ikiwepo kukwepa wajanja wanao chezea mashine lakini vile vile hali ya hatari yakupoteza mashine.” alisema Kibamba.

Katika wasilisho hilo lililopata wachangiaji wengi, Mkurugenzi Erick hakucha kuwashukuru wadau mbali mbali ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kutoa mawazo mbadala yakuboresha mifumo.

“Kufanya kazi  OR-TAMISEMI, haina maana ndio utakuwa unaelewa kila kitu, huu ni mpangilio tu wa majukumu, sisi kama wataalam ndani ya Wizara tunapokea mawazo yenye kujenga ili shabaha yetu yakuwahudumia wananchi iweze kufikiwa hivyo tunapokea mawazo yenye tija na kuyafanyia kazi kwa manufaa ya taifa” alisema Kitali.

Wasilisho hilo ambalo liliwasilishwa katika mkutano huo wa 34, lilihusiaha mifumo ya  Tovuti za Mikoa na Halmashauri (Government Website Framework GWF), ambao upo kwenye Halmashauri 185 na mikoa 26 nchini, mfumo wa Malipo unatumiwa na halmashauri (Epicor) na  mfumo wa Mipango na bajeti (Planning Budgeting and Reporting PlanRep).

Mifumo mingine iliyo wasilishwa katika kikao hicho ni Mfumo wa taarifa za Shule (School Information System SIS), mfumo wa Vibali vya kusafiria nje ya nchi (eVibali), Mfumo wa kukusanya, kuchambua na kutoa taarifa ya takwimu ya Elimu Msingi (Basic Education Management Information System BEMIS), Mfumo wa Uhasibu na Utoaji taarifa kwa ngazi ya kituo (Financial Facilities Account and Reporting System FFARS) pamoja na mfumo wa kukusanya, kuhifadhi na kutoa taarifa za kitabibu  (Government of Tanzania Health Management Information System GoTHoMIS).

Mkutano mkuu wa wa 34 wa Jumuiya ya Mamlaka za Mitaa ALAT,unafanyika mkoani Dodoma katika ukumbi wa Jakaya Kikwete na umewashirikisha Wenyeviti,Mameya, Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, watendaji kutoka OR-TAMISEMI pamoja na wadau mbali mbali wa maendeleo waliopata mialiko ya mkutano huo.

Erick Kitali Mkurugenzi wa TEHAMA, OR TAMISEMI, akiwasilisha mada kuhusu mifumo ya TEHAMA wanayo ihudumia na umuhimu wake katika juhudi za kusukuma maendeleo ya nchi. (Picha zote na Atley KuniOR TAMISEMI)
Wakili Kiomboni Kiburwa Kibamba, Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza akitchangia katika mada ya mifumo wakati wa mkutano wa 34 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa (ALAT) jijini Dodoma, 2018
Baadhi ya Wajumbe a Mkutano huo wa 34, wakisiliza kwa makini wasilisho la Mifumo inayosimamiwa na OR TAMISEMI.
Baadhi ya Wataalam kutoka Idara ya TEHAMA, wakiongozwa na Mkurugenzi msaidizi wa TEHAMA, Sutte Masuha wa kwanza kushoto, wakisiliza kwa makini hoja zilizo jitokeza wakati wa kikao cha 34 cha Jumuiya ya Tawala za Mitaa (ALAT), wakati wa uwasilishaji wa mada ya Mifumo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *