Habari za Wizara

Wakuu wa Shule za Umma Zilizong’aa Kidato cha Sita wapewa vyeti vya heshima

 

Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo, akizungumza kwenye halfa ya kuwapongeza Wakuu wa Shule za Sekondari za Umma 14 kati ya 30 zilizofanya vizuri katika matokeo ya kidato cha sita mwaka huu na kufanikiwa kuinga katika kumi bora kitaifa.

Zulfa Mfinanga na Aines Makassi,

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo leo amekabidhi vyeti vya heshima kwa Wakuu wa Shule za Sekondari za Umma 14 kati ya 30 zilizofanya vizuri katika matokeo ya mtihani wa kidato cha sita mwaka huu.

Akikabidhi vyeti hivyo leo Jijini Dodoma katika ukumbi wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI, katika kikao kazi cha tathmini ya matokeo ya mtihani wa Taifa wa kidato cha sita mwaka 2018, Mhe. Jafo amesema mafanikio hayo yanatokana na juhudi za wakuu hao wa shule pamoja na jitihada za serikali ya awamo ya tano iliyodhamiria kuinua ubora wa elimu nchini.

Mhe Jafo amesema hatua hiyo inatokana na mkakati uliowekwa na serikali wa kuhakikisha angalau shule tatu za serikali zinafanya vizuri na kuingia nafasi ya kumi bora katika matokeo ya kidato cha sita ambapo shule za sekondari Kibaha, Kisimiri na Mzumbe zimefanikiwa kuingia katika nafasi ya tatu bora.

“Kipindi cha nyuma wazazi walikuwa wanatamani sana watoto wao wasome katika shule za serikali, hali ikaja kubadilika baada ya shule hizo kukosa ubora, wazazi wakawa wanawapeleke watoto wao shule binafsi, lakini hivi sasa baada ya serikali kuwekeza kwenye shule za Umma, kila mtu anatamani watoto wao wasome shule za Umma” Alisema Mhe, Jafo.

Mbali na pongezi hizo pia Mhe jafo amewataka wakuu wote wa shule za serikali nchini kuhakikisha kuwa shule zisizopungua sita zinaingia katika nafasi ya kumi bora katika matokeo ya kidato cha sita mwakani pamoja na shule zisizopungua tano kuingia katika nafasi ya kumi bora katika matokeo ya kidato cha nne kuanzia mwaka 2020.

“Mmepitia changamoto nyingi hadi kufikia hapa lakini niwaombe mkitoka hapa kila mtu aende akagombee nafasi ya tatu bora, na tayari tumeweka mkakati wa kuhakikisha kuwa shule sita za umma zinaingia kumi bora katika matokeo ya kidato cha sita, na kuanzia mwaka 2020 shule tano za umma nazo zitaingia kumi bora katika matokeo ya kidato cha nne” Alielekeza Mhe, Jafo.

Kwa upande wake Mkuu wa shule ya sekondari Kisimiri ambayo kwa kwa muda wa miaka mitatu mfululizo imekuwa ikishika nafasi ya tatu bora nchini katika matokeo ya kidato cha sita, Mwl Valentine Tarimo ametaja siri ya mafanikio ni kufanya kazi kwa moyo na kusema licha ya shule hiyo kukabiliwa na changamoto mbalimbali lakini bado hazijawarudisha nyumba kiufaulu.

 “Shule yetu haina miundombinu ya barabara kuelekea shule, haina walimu walioajiriwa na serikali wa masomo ya fizikia na hisabati, waliopo tunawalipa kwa fedha za shule, pia hatuna fedha kwa ajili mahitaji mbalimbali, lakini mbali na changamoto hizo bado tunahakikisha kuwa tuafanya vizuri na kufikia malengo” Alisema Mwl Tarimo.

Hafla hiyo kwa wakuu wa shule zilizofanya vizuri katika matokeo ya kidato cha sita mwaka huu inatokana na agizo la Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Selemani Jafo kwa lengo la kuwatunuku vyeti vya heshima ambapo pia wakuu hao waliambatana na Makamu wakuu wasaidizi pamoja na walimu wa taaluma.

Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo, akimkabidhi cheti cha heshima Mkuu wa Shule ya Sekondari Kibaha, Chrisdom Ambikile katika hafla ya kuwapongeza Wakuu wa Shule za Umma zilizofanya vizuri katika mtihani wa kidato cha sita kitaifa mwaka huu.
Wakuu wa Shule, Makamu wakuu wa Shule na Walimu wa Taaluma waliohudhuria kwenye halfa ya kuwapongeza Wakuu wa Shule za Sekondari za Umma 14 kati ya 30 zilizofanya vizuri katika matokeo ya kidato cha sita mwaka huu na kufanikiwa kuinga katika kumi bora kitaifa wakimsikiliza Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo leo jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo, akimkabidhi cheti cha heshima Mkuu wa Shule ya Sekondari ya wasichana Tabora, Lidya Mwampamba katika hafla ya kuwapongeza Wakuu wa Shule za Umma zilizofanya vizuri katika mtihani wa kidato cha sita kitaifa mwaka huu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *