Wananchi Gairo Kupata Huduma Kwa Ukaribu.

Naibu Waziri Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI,  Selemani Jafo akizungumza katika uwekaji jiwe la msingi kwenye ujenzi wa jengo la Halmashauri ya wilaya ya Gairo mkoani Morogoro.

Na Atley Kuni- TAMISEMI

Kufuatia kuwekwa jiwe la msingi la ujenzi wa Halmashauri ya Gairo Mkoani Morogoro na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Sulemani Jafo (Mb) lililofikia asilimia 75 ya ujenzi ni ishara njema kuwa wananchi hao sasa watapata huduma kwa ukaribu tofauti na ilipokuwa hapa awali.

Ujenzi huo umetokana na agizo alilolitoa Agosti 17, mwaka huu, alipotembelea jengo la halmashauri ya Chamwino mkoani Dodoma na kuagiza halmashauri yeyote ambayo  ilipewa fedha za ujenzi wa Ofisi lakini zikashindwa  kuanza  ujenzi baada ya mwezi mmoja zingenyang’anywe fedha hizo na kupelekwa katika halmashauri ambazo wanaendele na ujenzi.

Naibu Waziri Jafo  akiwa katika ziara hiyo amewaagiza Makatibu Tawala wa mikoa yote nchini ambao halmashauri zao zilipatiwa fedha lakini bado hazijaanza ujenzi mpaka sasa wawasilishe majina ya halmashauri hizo kabla ya Oktoba 10, mwaka huu ili mchakato wa kuzihamisha fedha hizo ufanyike mara moja kwa kuzipeleka fedha hizo katika halmashauri zinazo endelea na ujenzi kwasasa.

 

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi Selemani Jafo akiweka jiwe la msingi katika jengo la Halmashauri ya wilaya ya Gairo mkoani Morogoro na kuagiza Makatibu Tawala wa Mikoa kuwasilisha majina ya Halmashauri ambazo hazijaanza ujenzi wake licha ya kuingiziwa fedha na serikali ifikapo Oktoba 10, mwaka huu ili mchakato wa kuzihamishia kwenye Halmashauri zenye uhitaji uanze mara moja.
Mbunge wa Jimbo la Gairo Ahmed Shabiby akizungumza na Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi) Selemani Jafo alipokuwa akikagua ujenzi wa jengo la Halmashauri ya Gairo

 

Akiwa katika Ziara hiyo Jafo hakusita kumnyooshea kidole Mkandarasi anayejenga barabara yenye urefu wa Km 3.5 ya Gairo Mjini kuhakikisha Barabara hiyo inakwenda sambamba na Ahadi za Ilani ya Chama cha mapinduzi ya 2015-2020, na kumtaka Meneja wa TARURA kusimamia ili ifikapo 2019 iwe imekamilika.

Awali akitoa taarifa ya ujenzi wa barabara hiyo mkandarasi Stephen Aloyce amesema ujenzi wa barabara hiyo umekamilika kwa asilimia 70 na kuiomba serikali kukamilisha malipo ya shilingi Bilioni 1.5 ili kumalizia kazi iliyobaki kabla ya kipindi cha mvua kuanza

Naibu Waziri Jafo, bado anaendele na ziara zake katika Mikoa na Mamlaka za Serikali Nchini kukagua shughuli mbali mbali za maendeleo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *