Habari za Wizara

Wananchi watakiwa kushiriki miradi ya Maendeleo

Naibu Katibu Mkuu –Afya, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Dkt. Dorothy Gwajima akikagua ramani ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Chamwino wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua utendaji kazi wa vituo vya afya vya Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino leo Jijini Dodoma.

Na Majid Abdulkarim.

Wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, katika kijiji cha Mlowa Barabarani wametakiwa kutoa ushirikikiano katika ujenzi wa Hospitali ya Wilaya hiyo ili kuleta maendeleo na kupunguza changamoto za afya nchini.

Hayo yamebainishwa na Naibu Katibu Mkuu Afya kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Dkt.Dorothy Gwajima wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua utendaji kazi wa vituo vya afya vya Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino Jijini Dodoma.

Dkt. Gwajima amesema kuwa Serikali pekee haiwezi kufanikiwa katika kuleta maendeleo bila kuwepo ushirikiano kutoka kwa wananchi wake hivyo ni vyema wananchi wakashirikishwa kikamilifu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini.

Amesema Serikali imejenga miundombinu ya afya nchini ikiwa na lengo la kuhakikisha huduma za afya zinaboreka kuanzia ngazi ya Zahanati, Vituo vya afya, Hospitali za Mikoa ili kupunguza changamoto katika sekta ya afya.

Akiendelea kufafanua amesema kuwa  wananchi wanatakiwa kuwa na dhamira ya dhati ya kusimamia  miradi ya ujenzi wa Hospitali za Wilaya    ili zijengwe  kwa ubora  kulingana na  fedha zilizotolewa na Serikali.

“Wananchi hakikisheni mnasiamia ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Chamwino kwa umakini mkubwa kwa kuangalia gharama zinazotumika zinaenda sambamba na majengo yanayojengwa kwa kuwa Hospitali hizi ni mali ya wananchi” Amesisistiza Gwajima

Akifafanua kuhusu ubora wa huduma zinazotolewa kwenye vituo vya afya amesema Serikali imejenga miudombinu ya afya nchini lakini bado changamoto kubwa ni watendaji waliopo katika vituo hivyo kutotimiza majukumu yao kwa uadilifu katika kutoa huduma bora kwa jamii hali ambayo inasababisha wananchi wengi kutokufika katika vituo hivyo.

“ Baadhi ya watoa huduma wamekuwa na lugha chafu kwa wateja, kutokuwa na ukarimu, kutowajibika kikamilifu, uzembe, rushwa ambapo  vitu vyote hivi vinapelekea wananchi kutokuja kutibiwa kwenye vituo vya afya vya Serikali na kukimbilia  vituo binafsi, naagiza watoa huduma wote nchini kuhakikisha wanafanyakazi kwa weledi katika kuwahudumia wananchi” Amesema Gwajima

Aidha amewataka wananchi kuhakikisha wanatoa taarifa pale wanapojibiwa vibaya na watoa huduma za afya nchini na Serikali haitasita kuwachukulia hatua za kinidhamu watumishi wote watakaobainika kuwa na makosa.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Chamwino, Athuman Masasi amesema kuwa watahakikisha wanakamilisha ujenzi wa Hospitali ya Wilaya hiyo kwa wakati ili wananchi waanze kupata huduma.

Naibu Katibu Mkuu –Afya, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Dkt. Dorothy Gwajima akikagua ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Chamwino iliyopo katika Kijiji cha Mlowa Barabarani wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua utendaji kazi wa vituo vya afya vya Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino leo Jijini Dodoma
Wananchi wa Mlowa Barabarani wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu –Afya, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Dkt. Dorothy Gwajima wakati akiongea na wananchi hao wkatika ziara ya kikazi ya kukagua utendaji kazi wa vituo vya afya vya Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino leo Jijini Dodoma
Naibu Katibu Mkuu –Afya, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Dkt. Dorothy Gwajima akikagua ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Chamwino iliyopo katika Kijiji cha Mlowa Barabarani wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua utendaji kazi wa vituo vya afya vya Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino leo Jijini Dodoma

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *