Afya

Wataalamu wa Mipango wapigwa msasa, Maandalizi ya Bajeti 2019/20

Majid Abdulkarim

Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia masuala ya Afya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Dk. Zainabu Chaula amewataka Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mikoa Sehemu ya Mipango na Uratibu sambamba na Maafisa Mipango wote wa Halmashauri nchini kutumia taaluma zao katika kukuza uchumi wa nchi ili kuleta matokeo chanya kwa jamii.

Dk, Chaula ameyasema hayo wakati  wa Ufunguzi wa Mafunzo ya Maandalizi ya Mipango na Bajeti katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa mwaka wa Fedha 2019/20 yanayofanyika kwa siku mbili Jijini Dodoma katika ukumbi wa Mikutano wa Royal Vilage Hoteli.

Dk. Chaula amesema mafunzo hayo ni fursa kwa maafisa hao kuhakikisha wanapata ujuzi na uelewa zaidi wa namna sahihi ya uandaaji wa Mipango na Bajeti katika Mikoa na Halmashauri.

“Ili kufikia matokeo bora ya kukuza uchumi wa nchi hii mnatakiwa kuwa wabunifu na kuhakikisha  mnabadilisha changamoto kuwa fursa kitu ambacho kitabadili dhana iliyopo kwa sasa kwa wananchi kulalamikia changamoto hizo na badala yake wazitumie kuwa fursa za kuwaletea maendeleo ” Alisema Dk. Chaula.

Aliongeza kuwa sisi wataalamu tupo hapa kwa niaba  ya wananchi hivyo tunatakiwa kuleta mipango itakayowezesha wananchi hao kujikwamua kiuchumi na kujiletea maendeleo endelevu na hili litafikiwa endepo mipango na bajeti inakwenda sambamba na fursa zinazopatikana katika maeneo yetu.

Aidha Dk. Chaula ameongeza kuwa kila mtumishi wa Umma anadhamana kubwa kwa taifa  na dhamana yenyewe ni kuhakikisha tunawatumikia vyema watanzania wenzetu ili kuleta matokeo bora kwa nchi yetu kama Muhasisi wa Taifa hili Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alivyo fanya na mpaka leo kupitia matokeo yake tunamkumbuka.

Aidha Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango OR-TAMISEMI Bw. John Cheyo, amesema kuwa kupitia mafunzo hayo maafisa hao watapata  uelewa aidi ya namna ya kuandaa bajeti iliyobora na halisi na zaidi watakuwa walimu wazuri kwa maafisa wengine katika maeneo yao ya kazi ambao hawajabahatika kupata mafunzo haya.

Naye Mkurugenzi wa Mradi wa Uimarishaji Mifumo ya Sekta ya Umma (PS3), Dk. Emanuel Malangalila amewataka  kuwa maafisa waliopata mafunzo haya  wakatumie wakatumie elimu hiyo  kuleta matokeo bora katika maeneo yao ya kazi ikiwemo kukuza uchumi na kupunguza umasikini katika mikoa na halmashauri zao.

Akihitimisha kwa neno la shukurani kwa niaba ya washiriki wenzake Katibu Tawala Msaidizi Mipango na Uratibu kutoka Mkoa wa Ruvuma Bw. Edmundi Godwell Siame amesema yote yaliyoelekezwa na viongozi kupitia ufunguzi wa mafunzo hayo sambamba na elimu watakayoipata katika mafunzo hayo watayazingatia na  kufanyia kazi ili kuhakikisha taaluma yao inakuwa nyenzo muhimu katika kukuza uchumi wa Nchi.