Video

Wauguzi Malampaka wasitishiwa safari za nje ya kituo

 Jengo la wodi ya wazazi na watoto lililojengwa katika Kituo cha afya cha Malampaka katika Halmashauri ya Wilaya ya Meatu Mkoani Simiyu.

Na. Angela Msimbira MASWA

Mratibu wa Mradi wa  Afya  ya Uzazi na Mtoto RMNCH-UNFPA na Huduma za Uuguzi na Ukunga  kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Bi.  Dinah Atinda amesitisha safari za nje ya kituo, mikutano, semina  na likizo kwa muda wa mwezi mmoja  kwa wauguzi wa Kituo cha Afya cha Malampaka katika Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Mkoani Simiyu.

Ametoa maagizo mara baada yakutembelea kituo hicho na kukuta huduma za afya zikiwemo za akina mama kujifungua zikifanywa na wahudumu wa afya (Medical Attendant) wakati wauguzi wote wakiwa kwenye semina  na mikutano mbalimbali jambo ambalo ni kinyume na utaratibu wa majukumu ya kazi.

“Ni hatari sana muhudumu wa afya (Medical Attendant) kuwahudumia wagonjwa akiwa peke yake bila usimamizi wa muuguzi kwa kuwa anaweza kusababisha madhara au kifo kwa mgonjwa na kushindwa kutoa maelezo sahihii juu ya chanzo cha kifo hicho” Amesema Bi. Atinda.

Bi. Atinda amefafanua kuwa jukumu la kuwahudumia wagonjwa katika Zahanati na Vituo vya afya ni la Wauguzi na Madaktari na si kazi ya wahudumu wa afya hivyo wanawafanya kutotimiza majukumu yao ya kufanya usafi wa mazingira na majengo.

Ameendelea kusema Serikali imetumia fedha nyingi katika kutengeneza miundombinu ya afya na vifaa na vifaa tiba  hivyo ni muhimu kila mmoja katika nafasi yake akatimiza majukumu ya kazi aliyopangiwa ili kutimiza lengo la kutoa huduma bora kwa jamii.

Amesema wauguzi ni kada  muhimu  na asilimia zaidi ya 80 ya huduma za afya nchini zinatolewa na wauguzi hivyo ni vyema wakafanyakazi  kwa weledi na kwakufuata misingi ya taaluma yao ili kutoa bora na kupunguza vifo vinavyoweza kuzulika kwa jamii.

 “Wauguzi mnao wajibu wa kutoa huduma kwa wananchi kwa kuzingatia kiapo na miiko ya taaluma yenu. Tunazo taarifa kuhusu baadhi ya wauguzi kutoa lugha chafu kwa wagonjwa, kutokuwepo kazini bila taarifa, kutokupanga utaratibu wa kazi (Roster) unaozingatia miongozo na kuwapanga wahudumu wa afya zamu bila wauguzi wenye ujuzi suala hili halikubaliki” Amesisitiza Bi. Atinda

Amesisitiza inasikitisha Kituo cha afya cha Malampaka kina watumishi 23 lakini  waliokutwa kazini ni 7 wwengine wakiwa kwenye ziara, mafunzo, semina na mikutano, hivyo kuzorotesha utoaji wa huduma za afya kwa jamii.

Wakati huohuo Bi. Atinda amesitisha safari, semina  mikutano na likizo  kwa muda wa mwezi mmoja  kwa Muuguzi Mkuu wa Mkoa, Muuguzi Mkuu wa Wilaya ya Maswa  na Mratibu wa afya ya uzazi na Mtoto wa Mkoa na Wilaya  na kuwataka kusimamia na kutatua changamoto zilizopo katika kituo hicho.

Amezitaka Timu za usimamizi wa Huduma za Afya za Mikoa na Wilaya  kuhakikisha  wanatimiza majukumu yao kwa kusimamia ujenzi wa vituo viwili vitakavyojengwa na kuhakikisha vituo vya kutolea huduma za afya  vilivyojengwa katika Mkoa wa Simiyu  vinaanza kufanyakazi.

Aidha amewataka waganga wafawidhi wa vituo kuhakikisha wanasimamia usafi, utendaji kazi na uwajibikaji wa watumishi ili vituo vya kutolea huduma za afya nchini vinaboreka na kuwavutia wananchi kuja kupata huduma hiyo.

Mratibu wa Mradi wa Afya ya Uzazi na Mtoto RMNCH-UNFPA na Huduma za Uuguzi na Ukunga kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Bi. Dinah Atinda akikagua kitabu cha utaratibu wa kazi (Roster) katika Kituo cha afya cha Malampaka katika Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Mkoani Simiyu
 Mratibu wa Mradi wa Afya ya Uzazi na Mtoto RMNCH-UNFPA na Huduma za Uuguzi na Ukunga kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Bi. Dinah Atinda akikagua jengo la wodi ya wazazi na watoto katika Kituo cha afya cha Malampaka katika Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Mkoani Simiyu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *