Habari za Wizara

Wauguzi wapongezwa, watakiwa kujipnaga kutoa huduma bora zaidi

Naibu Katibu Mkuu Afya, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Dkt, Dorothy Gwajima akipokelewa na wauguzi wakati akiwasili katika Hospitali ya Wilaya ya Iramba Mkoani Singida leo katika Maadhimisho ya sherehe za wauguzi nchini zilizofanyika Kiwilaya katika Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Mkoani Singida.

Na Angela Msimbira SINGIDA

Serikali imewapongeza wauguzi wote nchini na kuwataka kutoa huduma bora zaidi na kuhakikisha wanaleta mabadiliko makubwa ya ubora wa huduma za afya na kumaliza kabisa malalamiko kutoka kwa baadhi ya wateja huduma hususani kutokana na watumishi wachache wenye kauli zisizofariji.

Agizo hilo limetolewa katika Halmashauri ya Wilaya ya Iramba leo na Naibu Katibu Mkuu Afya, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Dkt. Dorothy Gwajima wakati wa maadhimisho ya siku ya wauguzi duniani yaliyofanyika Kiwilaya katika Hospitali ya Wilaya ya Iramba iliyopo  Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Mkoani Singida.

Amesema wauguzi nchini ni jeshi kubwa katika sekta ya afya kwa kuwa ndiyo wengi zaidi ukilinganisha na kada zingine hivyo, mnauwezo wa kuleta mabadiliko makubwa kwenye utoaji wa huduma bora kwa jamii iwapo wataamua kutumia taaluma zao kikamilifu.

Amesema wauguzi wakijitoa kwa wagonjwa na kuwahudumia kwa huruma na kuwajali kutasaidia kupunguza kero za afya nchini  na ubora wa huduma za kiuguzi ni muhimu katika kuwavutia watumiaji wa huduma kwani nyie ndiyo hukaa muda mwingi zaidi mteja.

 “kama ambavyo mmesema kwenye risala yenu kuwa, wauguzi wengi wanajitahidi kushika maadili ya fani ya uuguzi bali wachache wanatia dosari, nawaasa kutokukata tamaa na kutokuvunjika moyo bali waibueni wanaoharibu na wakataeni wasiojirekebisha msiwabembeleze kwa kuwa  , ni gharama kubwa kwa taifa kupoteza mteja mmoja sababu ya wauguzi wasio na maadili” Anasisitiza Dkt. Gwajima

Dkt. Gwajima amesema, kutokana na watumishi wachache wasiozingatia maadili ya taaluma za utumishi sekta ya afya wakiwemo matabibu, wauguzi na kada zingine zote, wateja wengi wanakuwa wanasita kuja vituoni kupata huduma na badala yake wanaishia kununua dawa na kunywa bila ushauri wa daktari ama wanaenda kutafuta huduma mbali zaidi kwa gharama kubwa zaidi na matokeo yake, wananchi wanakuwa wazito kujiunga na mifuko ya bima za afya.

 Dkt. Gwajima amesema tabia ya baadhi ya watoa huduma kukatisha tamaa wateja haikubaliki hivyo kila kituo kiwe na mifumo hai ya kupata maoni ya wateja ili kutoa fursa ya wasio na maadili kuibuliwa na jamii.

Ameendelea kueleza kuwa, wauguzi wanauwezo wa kufanya mageuzi katika Sekta ya afya  kwa kutoa huduma bora zaidi kwa jamii, kuacha lugha zisizofariji kwani huduma ya kwanza katika kituo cha afya ni lugha inayotumika na kauli ni kipimo cha wito wa utumishi.

Amesema kuwa, iwapo huduma zitatolewa kwa ubora unaostahili na raslimali zote kusimamiwa vizuri, wananchi wengi watajiunga na bima ya afya hivyo, itapunguza utegemezi wa vituo kwa serikali kuu katika kumudu gharama za uendeshaji huduma kila siku. Aidha, serikali itabaki inawezesha mambo makubwa yanayohusu miundombinu na ajira.

“haiwezekani tushindwe kutumia fursa ya bima ya afya katika kuboresha huduma kwa sababu tu, wapo baadhi wanakatisha tamaa kwa kukosa maadili. Aidha, haiwezekani wananchi  wajiunge na bima ya afya halafu washindwe kutumia huduma na fedha hizo zisirudi serikalini, lazima tujipange kwa huduma bora kuanzia kauli, uwepo wa vipimo, dawa na mazingira bora kwa ujumla”

Akielezea kuhusu kujitathmini katika utendaji kazi wa watoa Huduma za Afya Nchini Dkt. Gwajima amewataka wauguzi na watumishi wote wa sekta ya afya  kufanya ufuatiliaji na tathmini ya utendaji kazi kwa takwimu ili, kubaini uwingi wa kazi kwa kila mtumishi badala ya kutoa taarifa za ujumla jumla kuhusu upungufu wa watumishi.

“imeibuka tabia kila taarifa inayotolewa inataja upungufu wa watumishi lakini hakuna takwimu za uwingi wa kazi kwa watumishi waliopo sasa na unakuta baadhi ya vituo saa sita mchana wateja wameisha na ukichunguza zaidi utakuta hata baadhi ya watumishi waliopangwa zamu wengine hawakufika lakini ukiomba taarifa unaambiwa upungufu wa watumishi, je huwa tunachanganua kuwa hao waliopo huwa wamehudumia wateja wangapi tangu walipoingia kazini hadi wanatoka?”Amesema Dkt.Gwajima

Aidha amevitaka Vituo vya kutolea huduma kuwa, sambamba na kuboresha huduma wahakikishe wanaendelea kuwahamasisha wananchi kukata Bima ya afya ili kuondokana na utegemezi  kwa Serikali.

Wakati huohuo Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Iramba Dkt. Hussein Sekopo amesema katika mwaka wa fedha 2018/2019 jumla ya Kaya 9231 zimejiunga na Mfuko wa afya ya Jamii kati ya Kaya 15,000/= zilizotarajiwa sawa na asilimi 61.5 na jumla ya fedha zilizokusanywa ni zaidi ya shilingi milioni 92.

Naye Muuguzi Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Iramba Bi. NocklaVicent amewashukuru wauguzi wote kwa kufanyakazi kwa ushirikiano, upendo na weledi jambo ambalo limefanya sekta ya afya  kuendelea kuimarika

Aidha wameishukuru Serikali kwa kuajiri watumishi wapya wakiwemo wa Sekta ya Afya Nchini jambo ambalo limesaidia kupunguza uhaba wa watumishi  na kuboresha huduma kwa wananchi

Baadhi ya wauguzi wakiandamana katika maadhimisho ya siku ya wauguzi duniani iliyofanyika Kiwilaya katika Halmashauri ya Wilaya ya Iramba Mkoani Singida.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *