Afya

Wazee Chamwino Wakumbukwa Bima ya Afya

Diwani wa Kata ya Buigiri, Kenneth Yindi (Matonya) akionyesha mfano wa muonekano wa Kitambulisho cha matibabu ya wazee leo katika viwanja vya Ofisi ya Kata ya Buigiri Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma.

Na Fred Kibano

Kaimu Mkurugenzi Idara ya Afya, Huduma za Afya na Ustawi wa Jamii, Ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt. James Kengia, amekabidhi vitambulisho vya matibabu kwa wazee (VIP) katika hafla iliyofanyika katik viwanja vya Ofisi ya Kata ya Buigiri, Wilayani Chamwino mkoani Dodoma.

Kadi hizo zimekabidhiwa leo kwa wazee hao na Dkt. Kengia kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo, ikiwa ni moja ya jitihada zilizoanzishwa na Serikali ya Awamu ya Tano, chini ya Uongozi wa Mheshimiwa Rais John Magufuli katika kuboresha huduma za afya nchini.

 “Maeneo ambayo yalikuwa yanakosa huduma za afya kwa muda mrefu tumeanza ujenzi wa Vituo vya Afya vipya vya kimkakati, Zahanati mpya za kimkakati, lakini pia kwa zile zahanati au vituo vya afya vilivyokuwepo tumeanza kuvikarabati, na sio kuvikarabati tu, bali kuhakikisha kwamba tunapata huduma stahiki na kuongeza watumishi” alisema Dk. Kengia.

Naye Mhe. Mbunge wa Jimbo la Chilonwa, Wilaya ya Chamwino, Mhe. Joel Mwaka Makanyaga alitoa shukurani za dhati kwa Serikali ya Mhe. Rais Magufuli, pamoja na Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI, Selemani Jafo kwa neema hii.

“Namshukuru Mhe. Jafo kwani mwaka jana alitutengea milioni 500/- kwa kituo chetu cha afya cha Chamwino na kuweza kufanikisha hili, na kama haitoshi kupata vitambulisho vya matibabu kwa wazee wetu wa Chamwino” alisema Mhe. Makanyaga.

Baadhi ya wazee waliokabidhiwa vitambulisho hivyo kwa niaba ya wazee wengine kulingana na vijiji walivyotoka ndani ya kata hiyo ni Mzee Mikanoli Maloda wa Kijiji cha Chinangali 2 amesema wanaishukuru sana serikali kwa kuwajali na kutowasahau katika huduma hii muhimu ya kijamii kwani sasa wanauhakika na matibabu.

“Tumefurahi sana kupitia serikali ya awamu ya tano kwani sisi wazee tunapata matatizo sana kutokana na hali duni ya fedha, hivyo hivi vitambulisho vitatusaidia kuweza kupata matibabu kwa haraka na uhakika” alisema Mzee Maloda.

Kwa upande wake Kiongozi wa Kundi la Wazalendo kutoka Vyuo Vikuu Dkt. Seni Msuya wa Chuo Kikuu cha Dodoma amekumbushia maadui watatu aliowakataa Baba wa Taifa Mwl Julius Kambarage Nyerere, ambao ni ‘Umasikini, Ujinga na Maradhi’ na ndio maana Serikali ya Awamu ya Tano imefanya jitihada kuhakikisha leo wazee mmepata Vitambulisho vya matibabu kwa wazee.

Ikumbukwe kuwa kila ifikapo tarehe 14 Octoba ya kila mwaka, watanzania huadhimisha kifo cha Baba wa Taifa la Tanzania,Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambaye kifo chake kilitokea tarehe 14 Octoba 1999.

Utaratibu huu wa utoaji wa vitambulisho kwa wazee umeratibiwa na OR-TAMISEMI, Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, Mbunge wa Jimbo la Chilonwa kwa kushirikiana na Diwani wa Kata ya Buigiri.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *