Habari Kitaifa

Waziri Jafo, Aongoza Mawaziri utatuzi wa Mgogoro wa Hifadhi Makere kusini

Waziri wa Nchi OR TAMISEMI, Mhe. Seleman Jafo alipokuwa akiongza kikao hicho cha Mawaziri kutoka Sekta tofauti tofauti kuhusiana na utatuzi wa mgogoro wa hifadhi Makere kusini

Mawaziri watano wakioongozwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Suleiman Jafo, wamekagua hifadhi ya  Msitu  wa Makere Kusini  uliopo wilaya ya Kasulu mkoa wa Kigoma kwa takriban saa tano ili kubaini changamoto mbalimbali za msitu huo na kuzipatia ufumbuzi.

Mawaziri wengingine mbali ya Mhe. Seleman Jafo, ni Waziri wa Maliasili na Utalii Dk Hamis Kigwangala, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk. Angeline Mabula pamoja na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira Musa Sima.

Ziara ya mawaziri hao katika hifadhi ya msitu huo ambao pia unatambulika kama Msitu wa Kagera Nkanda ambao niwa kihistoria kutokea hapa nchini ilianza majira ya saa saba mchana jana wakati Mawaziri hao walipokuwa wakitokea wilayani Kigoma ambapo walikuwa na kikao cha utatuzi wa mgogoro wa matumizi ya ardhi katika hifadhi ya Msitu na Pori la Akiba la Moyowosi la mkoani Kigoma na kumalizika kwa ukaguzi majira ya saa kumi na mbili jioni.

Baada ya kumalizika kwa ukaguzi katika Msitu wa Makere Kusini, Mawaziri hao watano walielekea kijiji cha Kabulanzwili na kukagua mpaka baina ya kijiji hicho na hifadhi ya msitu huo kwenye mto Migezibiri na baadaye kukutana na wananchi wa kijiji hicho kwa lengo la kuwaeleza nia ya serikali kunusuru hifadhi ya msitu ambapo walizungumza nao hadi saa moja na nusu usiku.

Wakiwa katika kijiji cha Kabulanzwili waliwapokelewa na wananchi walikuwa na   mabango huku wananchi wakionesha kutoridhishwa na hatua zinazochukuliwa na askari wa wanyama pori katika eneo hilo kwa kuwaondoa kwa nguvu wananchi wanaoendesha shughuli za kilimo na ufugaji kwenye hifadhi hiyo, huku baadhi yao wakidai kutofahamu mipaka halisi baina ya kijiji na hifadhi katika eneo hilo.

Ziara ya viongozi hao ilikwenda sambamba na kufikia maazimio tisa kwa ajili yakunusuru misitu lakini pia kumaliza migogoro iliyokuwepo baina ya serikali na wananchi hao, maazimio yaliyofikiwa ni pamoja na;

Serikali itaendesha Operesheni kubwa kuondoa uvamizi wa wakulima, wafugaji na watu wengine wanaofanya shughuli zisizo halali kwenye misitu na mapori yaliyohifadhiwa kisheria zikiwemo hifadhi za misitu ya serikali kuu, hifadhi za misitu za halmashauri za wilaya na vijiji. Hivyo, wavamizi wote wanaoishi au kuendesha shughuli zozote kwenye mapori na misitu hiyo waondoke mara moja kwa hiyari kabla ya zoezi la kuwaondoa kwa lazima. Operesheni hiyo itafanyika wakati wowote ndani ya kipindi cha miezi sita (6) kuanzia Januari 2019. Hata hivyo, imeshauriwa kwa wakulima ambao tayari wana mazao katika mapori na hifadhi husika wanaweza kuomba idhini maalum ya kuvuna mazao yao.

Azimio linguine ni kwamba, Serikali imemega jumla ya hekta 10,012.61 kutoka kwenye Hifadhi ya Msitu wa Makere Kusini kwa ajili ya kilimo na mipango ya Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu ambapo Hekta 2,174 (ekari 5,435) zimetolewa kwa Kijiji cha Mvinza, Hekta 2,496 (ekari 6,240) zimetolewa kwa Kijiji cha Kagerankanda na Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu Hekta 5,342.61 (ekari 13,356.525). Eneo hili lilitolewa na Mhe. Rais ili litumike kwa ajili ya shughuli za kilimo na ufugaji. Serikali itaandaa mpango mahsusi wa matumizi bora ya ardhi ili kuwezesha zoezi la ugawaji kufanyika vizuri.

Taarifa iliyotolewa kwa umma imesema, Wizara ya Mifugo na Uvuvi imetenga jumla ya hekta 20,000 kutoka katika maeneo mbalimbali katika Mkoa wa Kigoma kwa ajili ya ufugaji wenye tija aidha serikali itaendelea kutafuta maeneo mengine kwa ufugaji wenye tija.

Ilikuweka kuwa na msimamo wa pamoja Serikali imesisitiza kuimarisha utekelezaji wa sheria zinazohusu wakimbizi ili kuhakikisha hawachangii uharibifu wa mazingira, maliasili na usalama;

Maazimio mengine ni kuwa ilibainika wahamiaji haramu kutoka nje ya nchi wamekuwa wakichangia katika uharibifu wa misitu na mapori hivyo serikali imesema wahamiaji hao haramu wataondolewa nchini mara moja kwa kutumia sharia za nchi zilizopo.

Serikali imesema pia wananchi wote waliovamia eneo lililoko kwenye mpango wa uanzishwaji wa vitalu vya ufugaji na mashamba ya kilimo katika Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza (Mwanduhubanhu) watapangwa na mamlaka husika kwa ufugaji na kilimo chenye tija, mara baada ya tathimini iliyoelekezwa na Waziri wa Mifugo kukamilika;

Sambamba na hayo hapo juu, Serikali itasaidia vijiji katika maeneo yao kuandaa mipango ya matumizi bora ya ardhi na katika mipango hiyo watenge maeneo kwa ajili ya ufugaji na kilimo kulingana na mahitaji yao;

Katika hatua nyingine maazimio hayo ya serikali kupitia Mwaziri wake, imesema, Mamlaka za Serikali za Mitaa zenye mashamba ambayo hayajaendelezwa zihakikishe taratibu za ubatilisho wa miliki hizo umefanyika ili ardhi itakayopatikana ipangwe kwa matumizi ya kilimo na ufugaji wenye tija huku iki utaka uongozi wa Mkoa na Wilaya uhakikishe kuwa usafirishaji wa mifugo unazingatia Sheria ya Utambuzi, Usajili na Ufuatiliaji wa Mifugo Na. 12 ya mwaka 2010.

Hii ni mara ya kwanza kwa Wizara hizo kukutana mkoani humo na kutafuta suluhu ya migogo ya hifadhi hapa nchini.

 

 

Waziri Jafo akiwa anawaongoza Mawaziri wenzake katika ziara yakukagua Msitu huo

Wananchi wakiwa katika hali ya usikivu huku wakiwasiliza Mawaziri hao kwa makini waliofika kwa ajili yakuzungumza nao, Mawaziri hawapo pichani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *