Elimu

Zoezi la Kubaini Watoto wenye Mahitaji Maalum nchini Lafanikiwa

Na. Fred Kibano- TAMISEMI

Zoezi la kuwabaini watoto wenye mahitaji maalum chini ya Mpango wa kukuza stadi za kujua Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) linaloendeshwa na Ofisi ya Rais TAMISEMI ambalo lilianza wiki tatu zilizopita ni la mafanikio makubwa.

Akiongea mjini Morogoro wakati wa kikao na timu ya kubaini watoto hao kwa mkoa wa Morogoro, Mratibu wa Mpango huo kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Julius Migea amesema zoezi hilo limeisaidia Serikali kupata takwimu na mahitaji ya watu wenye mahitaji maalum na hivyo kilio cha watoto hao na watu wenye mahitaji maalum kitafikishwa Serikalini ili kuzipatia ufumbuzi.

Amesema Serikali inatambua vema kilio cha watoto hao na ndio maana imetenga fedha kwa ajili ya kuendesha zoezi hilo nchi nzima ili kuwabani na kuweka mipango yake kwa ajili ya watoto wenye mahitaji maalum.

Kiongozi wa kikosi kazi cha kubaini watoto wenye mahitaji maalum mkoa wa Morogoro, Stephen Msome ambaye ni Afisa Elimu – Elimu Maalum Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero, amesema zoezi hilo mkoani humo limekuwa na mafanikio makubwa licha ya kukumbana na changamotokadhaa.

“zoezi la kuwabaini watoto wenye mahitaji maalum limefaulu kwa ushindi mkubwa sana, wazazi wamejitokeza kwa wingi kuwaleta watoto wenye mahitaji maalum na hata wale waliokuwa wamefichwa wameweza kuletwa na tumeweza kuwabaini pamoja na changamoto walizonazo, wazazi wamefurahia zoezi wameona Serikali imewakumbuka”

Msome amesema katika mkoa wa Morogoro zoezi hili limeendeshwa katika Halmashauri zipatazo tisa ambazo ni pamoja na Malinyi, Ulanga, Kilombero, Kilosa, Ifakara, Gairo, Mvomero, Halmashauri ya Wilaya Morogoro na Morogoro Manispaa.

“tumekumbana na changamoto mbalimbali mojawapo ikiwa ni baadhi ya wazazi kuendelea kuwaficha watoto kwa ajili ya kubainiwa, pia wazazi kukaa mbali na vituo vya kutolea huduma kama vile mashule, zahanati, vijiji na hii imesababisha zoezi la huduma kushindwa kuwafikia kule walipo kutokana na hali mbali ya hewa”

Msome amesema wamefanya zoezi la kuwabaini watoto hao wenye mahitaji maalum na kuwashauri kama vile kuwaandikisha watoto mashuleni, kujiunga na vituo vinavyotoa huduma kwa watoto walemavu, kujiunga na shule jumuishi ili kuendelea na masomo yao.

zoezi hili lililofanyika nchi nzima limedumu kwa muda wa takribani wiki tatu ambalo limekuwa na mafanikio makubwa katika kuwabaini watoto wenye mahitaji maalum kuanzia umri wa miaka 4 hadi sita, lakini pia kuwashauri wazazi mahali ambapo huduma nyingi za kielimu. kitabibu na kijamii zinapatikana ili kuwafaya watoto hao kusoma na kuweza kujitegemea.

Mbainishaji wa watoto wenye mahitaji maalum Stephen Msome akitoa huduma ya mazoezi kwa mtoto Swaumu Ramadhani wakati wa zoezi hilo mjini Morogoro leo.
Mratibu wa Mpango wa Stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Julius Migea (wa kwanza kulia) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wajumbe wa timu kazi ya mkoa wa Morogoro waliofanya zoezi la kuwabaini watoto wenye mahitaji maalum mkoani Morogoro

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *